| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mahakama ya juu ya DRC yaruhusu mchakato ambao utampa nafasi Tshisekedi kugombea muhula wa tatu
Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wiki hii iliidhinisha mapendekezo ambayo yanaweza kumpa nafasi Rais Felix Tshisekedi kugombea muhula wa tatu baada ya kura ya maoni.
Mahakama ya juu ya DRC yaruhusu mchakato ambao utampa nafasi Tshisekedi kugombea muhula wa tatu
Rais wa DRC Felix Tshisekedi anasema yuko tayari kugombea muhula wa tatu kama raia watamtaka afanye hivyo.

Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wiki hii iliidhinisha mapendekezo ambayo yanaweza kumpa nafasi Rais Felix Tshisekedi kugombea muhula wa tatu baada ya kura ya maoni.

Tshisekedi, 63, amekuwa madarakani tangu 2019 na kulingana na katiba ya sasa anaruhusiwa kuongoza kwa mihula miwili pekee wakati kipindi chake cha miaka mitano ya pili kitakapomalizika mwishoni mwa 2028.

Kwa miezi kadhaa kiongozi huyo wa nchi na wanaomuunga mkono wamekuwa wakijiandaa kwa kura ya maoni, bila kusema wazi kuwa atagombea muhula wa tatu.

Tshisekedi yuko tayari kwa muhula wa tatu

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mapema mwezi Mei, Tshisekedi alisisitiza kuwa "hatowania muhula wa tatu" lakini akaeleza: "Kama watu watamuomba agombee muhula wa tatu, basi atakubali."

Katiba ya DRC ya sasa inaruhusu mihula miwili tu kwa rais na kusisistiza kuwa haiwezi kufanyiwa marekebisho.

Muswada ulioidhinishwa siku ya Jumanne na mahakama ya katiba utafanya iwe rahisi kubadilisha vifungu vya katiba, iwapo rais ataagiza mchakato huo.

Ili kufanya hivyo, kiongozi huyo wa nchi itabidi ateue jopo la wataalamu ambalo mapendekezo yake yatawasilishwa bungeni.

Kura ya maoni

Bunge hilo linaweza kuidhinisha kwa wingi wa humusi tatu, kabla ya raia kuupigia kura muswada huo.

Katiba mpya huenda pia ikaanzisha upya muhula wa urais kwa Tshisekedi.

Juni 12, raia waliokuwa wanapinga muswada huo waliandamana katika barabara za mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kinshasa.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili