| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Sudan yatoa wito kwa raia walioko nje kurudi nyumbani
Serikali inasema hatua hii ni sehemu ya mpango mpana kuhamasisha raia wa Sudan walioondoka katika makazi yao kurudi na kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Sudan yatoa wito kwa raia walioko nje kurudi nyumbani
Sudan imetoa shukrani zake kwa Misri kwa kuwapokea mamilioni ya raia wa Sudan. / Wengine
tokea masaa 3

Sudan imetoa wito kwa raia walioondoka katika makazi yao na wanaoishi nje ya nchi kurudi nyumbani, huku serikali ikiimarisha hatua za watu kurudi kwa hiari na kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanaorudi nyumbani.

Waziri Mkuu Kamil Idris amesema ofisi yake ina dhamira ya kufanya iwe rahisi kwa watu kurudi na kuhakikisha kuwa raia watapata nafasi ya kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa nchi, shirika la habari la umma SUNA limeripoti.

Akizungumza wakati alipotembelea mpaka wa Ashkeit huko Wadi Halfa siku ya Jumanne, Idris alisema mamlaka zimechukua hatua za kuondoa kodi zisizo halali na kuhakikisha kuwa raia wanaorudi hawakabiliwi na suala la malipo zaidi, kodi za lazima au ushuru wa forodha. Alieleza kuwa hali kama hiyo imekuwa mzingo kwa raia bila kufaidi nchi.

Waziri Mkuu anasema serikali inajitahidi kuimarisha mazingira katika maeneo muhimu ya mipaka ya kuingia nchini, akiagiza Wizara ya Fedha kutatua changamoto za umeme katika mipaka hiyo na kuahidi kuleta vifaa vya kufanya ukaguzi. Pia aliagiza kufanyike kwa tathmini kamili ya upatikanaji wa maji na kutoa wito wa ushirikiano kati ya mamlaka za afya na maafisa wa mpakani kutatua masuala tata.

Msaada wa kimataifa

Sudan pia ilitoa shukrani zake kwa Misri kwa kuwapokea mamilioni ya raia wa Sudan na kusaidia katika kurudi nyumbani kwa hiari.

Mamlaka za serikali ya mitaa zinasema raia wanaourdi watapata usaidizi kuhakikisha wanarudi salama. Serikali ya Jimbo la Kaskazini ilieleza kuwa iko tayari kusaidia wanaorudi nyumbani.

Idris amesema kivuko cha Ashkeit kiko tayari kwa ajili ya raia wanaorudi, akiongeza kuwa utaratibu wa forodha na hati za kusafiria unaendelea vizuri. Pia alikutana na raia katika kivuko hicho, kusikiliza kero zao na kuwaamuru maafisa kutatua kero hizo.

Zaidi ya watu 40,000 wameuawa katika kipindi cha miaka mitatu iliopita, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa. Mashirika ya misaada yanasema idadi halisi ya waliouawa inaweza kuwa juu zaidi.

CHANZO:TRT Afrika and agencies