Uturuki kuruhusu viza bila malipo kwa raia wa China

Kuanzia Januari 2, raia wa China wenye hati za kusafiria za kawaida wanaweza kutembelea Uturuki kwa hadi siku 90 bila viza, hatua inayolenga kuimarisha utalii na uhusiano wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

By
Hatua hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. / Reuters

Uturuki imewaruhusu rasmi raia wa China wenye hati za kusafiria za kawaida kuingia bila viza kwa ajili ya utalii na usafiri wa muda mfupi, kwa mujibu wa tamko la Rais lililochapishwa katika Gazeti la serikali Jumatano.

Sera mpya, iliyosainiwa na Rais Recep Tayyip Erdogan, inawawezesha raia kutoka China kukaa Uturuki hadi siku 90 ndani ya kipindi cha siku 180, na sera hiyo itaanza kutumika kuanzia tarehe 2 Januari 2026.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha utalii na biashara kati ya mataifa hayo, hii inafuatia ongezeko kubwa la wageni kutoka China.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Uturuki, takriban watalii 410,000 kutoka China walitembelea Uturuki mwaka 2024, ongezeko la asilimia 65.1 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Sasa China imekuwa moja ya masoko yanayokua kwa kasi kwa ajili ya utalii wa Uturuki.

Vivutio vinavyotambulika kimataifa

Mwanzoni mwa mwaka huu, Balozi wa China Jiang Xuebin alisisitiza kuwa wasafiri kutoka China wanavutiwa na Uturuki.

"Uturuki huwavutia watalii wa China kutokana na utajiri wake wa historia, utamaduni wake, na vivutio vinavyotambulika duniani," alisema katika tukio la Ubalozi wa China mjini Ankara. "Kipindi baada ya janga la corona kimeonesha ongezeko la kushangaza la idadi ya wageni, na Uturuki imekuwa soko linalokua kwa kasi zaidi miongoni mwa wageni wa kimataifa."

Balozi Jiang alibainisha kwamba amekuwa shahidi wa ustaarabu wa kale na maajabu ya asili ya nchi hiyo, jambo linalosisitiza kuongezeka kwa uhusiano wa kitamaduni na utalii kati ya mataifa hayo.

Hatua hiyo inatarajiwa kukuza zaidi utalii wa Wachina, kusaidia uchumi wa ndani, na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Uhusiano kati ya Uturuki na China unaimarika kupitia upanuzi wa biashara, utalii, na ubadilishanaji wa kitamaduni, huku pande zote mbili zikichukua hatua za kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia.