Rais wa Marekani Donald Trump atahudhuria mkutano wa viongozi wa nchi za NATO jijini Ankara mwezi Julai, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema.
Rubio alisema siku ya Jumatano kuwa mkutano huo utakuwa "mkutano muhimu sana" katika historia ya muungano huo kwa sababu "kuna baadhi ya masuala yanayotakiwa kuangaziwa na kutatuliwa."
“Marekani bado ipo ndani ya muungano wa NATO, na itakuwepo," Rubio ameiambia Kamati ya Bunge kuhusu Mambo ya Nje.
Huku Marekani ikiwa bado ni wanachama, alisema shirika hilo linahitaji "mabadiliko muhimu" ambayo yatajadiliwa kwenye kongamano hilo la Julai 7-8 mji mkuu wa Uturuki.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan siku ya Jumanne pia alieleza kuhusu mipango ya Trump kuhudhuria mkutano wa NATO.
Alisema Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amezungumza na Trump mara kadhaa kwa njia ya simu mwezi uliopita na kwamba raia wa Marekani ameeleza kila mara kuwa atakuwepo kwenye mkutano huo.
Akisisitiza kuwa Marekani bado iko thabiti kwenye muungano huo licha ya matamshi ya kisiasa, Fidan amesema hakuna dalili kuwa Marekani ina mpango wa kujiondoa katika NATO.
“Marekani imekuwa ikishinikiza washirika kuongeza matumizi katika masuala ya kijeshi na kuchukua majukumu ya usalama wao wenyewe,” alieleza, akifafanua kuwa:
“Mataifa ya Ulaya yamepokea ujumbe huo na tayari yamechukua hatua za kuongeza bajeti zao za kijeshi ndani ya NATO.”
“Wakati viongozi wanapokuja pamoja, tutatathmini maendeleo yaliyofikiwa,” alisema.




















