| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Kenya haitasafirisha madini ghafi tena: Rais Ruto
Ruto alisisitiza kuwa Kenya itawekeza katika kuboresha uwezo, kuvutia ushirikiano wa viwanda, na kuanzisha motisha za sera ili kusaidia usindikaji wa ndani.
Kenya haitasafirisha madini ghafi tena: Rais Ruto
''Vizazi vijavyo vitatuuliza, kulikuwa na Titanium nchini Kenya ilikwenda wapi ? Na hatutakuwa na jibu' asema Rais Ruto / Others

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kwamba Kenya haitauza tena madini ghafi, jambo linaloashiria mabadiliko makubwa katika sera ya rasilimali ya nchi inayolenga kukuza viwanda vya ndani na kuongeza faida za kiuchumi.

Akiongea katika Kongamano la ‘Afrika We Build’ jijini Nairobi, Ruto alisema enzi ya usafirishaji wa maliasili ambayo haijachakatwa nje ya nchi lazima ifikie kikomo, akisema kuwa tabia hiyo kihistoria imeinyima Kenya kazi, uhamishaji wa teknolojia na mapato ya juu.

Badala yake, serikali itaweka kipaumbele kwenye manufaa ya ndani, kuchakata madini ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

‘Kumbuka tulikuwa na Base Titanium, mojawapo ya makampuni ambayo yalikuwa yakisafirisha Titanium nje ya Kenya. Walisafirisha kila kitu, wakafunga migodi na hatukupata chochote,’’ Rais Ruto alisema.

Wajibu kwa vizazi vijavyo

Ruto aliongeza kuwa vizazi vijavyo vitawawajibisha kwa rasilimali zilizopotea.

‘Vizazi vijavyo vitatuuliza, kulikuwa na Titanium nchini Kenya ilikwenda wapi? Na hatutakuwa na majibu. Ndio maana kusonga mbele, ardhi yetu , dhahabu yote na madini mengine yote, hatutazisafirisha zikiwa ghafi tena.’’

Hatua hiyo inalinganisha Kenya na idadi inayoongezeka ya mataifa tajiri kwa rasilimali yanayotaka kuhifadhi thamani zaidi kutoka kwa mali zao asilia.

Nchi nyingi barani Afrika zimezidi kusukuma sera zinazofanana, hasa katika sekta kama vile ardhi adimu, dhahabu, na madini muhimu kwa mpito wa nishati duniani.

Ruto alisisitiza kuwa Kenya itawekeza katika kuboresha uwezo, kuvutia ushirikiano wa viwanda, na kuanzisha motisha za sera ili kusaidia usindikaji wa ndani.

Mkakati huo unatarajiwa kuathiri madini muhimu kama vile titanium, soda ash, madini mapy yaliyogunduliwa na madini adimu za dunia.

CHANZO:TRT Afrika Swahili