Misri imesema iko tayari kupokea wagonjwa kutoka Gaza Mpaka wa Rafah utakapofunguliwa

Gavana wa Kaskazini mwa Sinai Meja Jenerali Khaled Mujawir ameiambia televisheni ya taifa Jumatano kwamba upande wa Misri wa mpaka wa Rafah umejiandaa kwa kitakachojiri.

By
Misri imesema iwapo Mpaka wa Rafah utafunguliwa, basi itakuwa tayari kupokea majeruhi kutoka Gaza. / Reuters / Reuters

Misri imesema iko tayari kupokea majeruhi kutoka Gaza na kupeleka misaada ya kibinadamu katika eneo hilo lililozingirwa punde tu Mpaka wa Rafah utakapofunguliwa.

Gavana wa Kaskazini mwa Sinai Meja Jenerali Khaled Mujawir ameiambia televisheni ya taifa Jumatano kwamba upande wa Misri wa mpaka wa Rafah umejiandaa kwa kitakachojiri.

“Kituo cha kukabiliana na migogoro kinatathmini hali zote, ikiwemo kupeleka misaada, iwapo hali itaruhusu, katika maandalizi ya kufunguliwa kwa mpaka," amesema Mujawir.

Amesema kwamba Misri imefanya maandalizi, na kusisitiza kwamba uratibu unaendelea mjini Cairo na taasisi zote za serikali.

“Tuko tayari asilimia 100 kuingizwa kwa misaada na kupokea majeruhi kutoka Gaza.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari za Serikali ya Israel KAN, mpaka wa Rafah unatarajiwa kufunguliwa pande zote Februari 1.

Utekelezaji wa sharti la kwanza

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza Oktoba 9, 2025, kwamba Israel na Hamas wamepitisha hatua ya kwanza ya mpango wa usitishaji wa mapigano katika majadiliano yaliyokuwa yakiendelea Misri.

Utekelezaji wa usitishaji wa mapigano ulianza siku ya pili, kufuatia kupitishwa na serikali ya Israel.

Mwili wa teka wa mwisho wa Israel Ran Gvili uliokuwa Gaza umepatikana na kurudishwa Israel Januari 26, huku makundi makubwa ya Wapalestina Gaza yakitekeleza makubaliano ya awamu ya kwanza.

Licha ya usitishaji wa mapigano, jeshi la Israel limekuwa likiendelea kuwashambulia Wapalestina Gaza.

Wakati huo huo, balozi wa Trump wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff ametangaza Januari 14 awamu ya pili ya vipengele 20 vya Kamati ya Kitaifa ya Utawala wa Gaza inayojumuisha wataalamu wa Kipalestina imeundwa chini ya uongozi wa Ali Shaath, kuongoza eneo hilo.

Kufunguliwa tena kwa mpaka wa Rafah, ambao ulifungwa na Israel tangu Mei 2024, na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya awali.