TRT yaondoka mkutano wa EBU wakati wanachama wakitofautiana kuhusu ushiriki wa Israel Eurovision

Vyombo vya habari vilishutumu kuendelea kushiriki kwa Israel huku mauaji ya halaiki yakiendelea Gaza, wanachama kadhaa wa bara Ulaya walitangaza kususia mashindano ya Eurovision 2026.

By
Wajumbe wametofautiana kuhusu ushiriki wa Israel huku mauaji ya halaiki Gaza yakijadiliwa katika mkutano wa EBU. / Reuters

Mkutano Mkuu wa 95 wa Muungano wa Vyombo vya Habari barani Ulaya (EBU) jijini uligubikwa na mjadala kuhusu nafasi ya Israel kwenye mashindano ya kuimba ya Eurovision, huku wanachama wakijadili kuhusu sheria mpya za ushiriki na hadhi ya shirika la utangazaji wa umma la Israel KAN kwa ajili ya 2026.

Kabla kura kuanza kupigwa, wanachama walizungumzia kama ushiriki wa KAN unatakiwa kuendelea huku Israel ikiendeleza mauaji ya halaiki huko Gaza.

Wakizungumza kama wanachama waasisi wa EBU, Shirika mama la TRT World, TRT walisema hali huko Gaza inafanya ushiriki wa Israel kutoenda sawa na maadili ya Eurovision.

"Kama watu wengine wote katika ukumbi huu, sisi hapa TRT tumeshuhudia mateso na mauaji ya halaiki ya miongo kadhaa yakitokea huku dunia ikitizama," ujumbe huo ulisema.

"Tangu usitishwaji mapigano kuanza, watoto kadhaa wameuawa na misaada haiwezi kufika Gaza salama. Waandishi wa habari zaidi ya 270 wameuawa na Israel. Msimamo wetu uko wazi: kuruhusu KAN kushiriki si sahihi na hakuendani na maadili ya mashindano haya."

Nchi zaidi zinasusia

Shirika la Ireland la RTÉ liliunga mkono misimamo huo, likisema: "Kufuatia mauaji mabaya huko Gaza na hali mbaya kwa watu inayoendelea, tunaamini haitokuwa sawa kwa KAN ya Israel kuendelea kuwepo kwenye mashindano."

Wakati shirika hilo la habari la Israel lilipoanza kuzungumza, wawakilishi wa TRT waliondoka ukumbini kwa kususia.

TRT na wanachama wengine walipinga upigaji kura wa wazi na kutaka kufanyike kura ya siri.

Mwishowe, Mkutano huo uliidhinisha sheria mpya za ushiriki lakini ikaamua kutopiga kura mahsusi kuhusu ushiriki wa Israel.

Wanachama wa Ujerumani na Austria walieleza wazi kuwaunga mkono KAN, huku wanachama kutoka Uhispania, Slovenia, Ireland na Uholanzi wakitangaza baada ya kura kuwa watasusia Eurovision 2026.

Kutofautiana huko kumekuja huku vita vya Israel dhidi ya Gaza vikiendelea licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitishwa mapigano yaliyotaratibiwa na Marekani, na Wapalestina wakiendelea kuuawa na shutuma za kimataifa zikijitokeza kutoka taasisi zote za kitamaduni, kisiasa na vyombo vya habari.