| Swahili
UTURUKI
4 dk kusoma
Uturuki inazitaka jamii za Kiislamu kudhibiti upya simulizi zao wenyewe
Duran anasema migogoro haiishi tu katika uwanja wa vita pekee, bali pia inapiganwa kwa kuunda na kudhibiti mitazamo pamoja na taarifa.
Uturuki inazitaka jamii za Kiislamu kudhibiti upya simulizi zao wenyewe
Duran alielezea matumaini kwamba mazungumzo na ushirikiano unaoendelezwa katika jukwaa hilo utaimarisha umoja katika ulimwengu wa Kiislamu. / AA / AA

Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran, amezitaka jamii za Kiislamu kudhibiti upya simulizi zao wenyewe, akionya kuwa mfumo wa kimataifa unakabiliwa na changamoto kubwa za kukubalika na kuaminika, na kwamba wale walioujenga mfumo huo sasa ni miongoni mwa wanaouchangia kuudhoofisha.

Akizungumza katika Jukwaa la Muslim Impact Forum 2026 lililofanyika mjini Istanbul, Duran alisema dunia inapitia mabadiliko makubwa ya kihistoria katika miongo iliyopita.

“Vita, mauaji ya kimbari, majanga na kukosekana kwa imani katika taasisi na kanuni za kimataifa vinaonyesha wazi kwamba mpaka muhimu umeshavukwa,” alisema, akiongeza kuwa jumuiya ya kimataifa haina dira iliyo wazi ya mustakabali wake.

Duran alibainisha kile alichokiita viashiria vya msingi vya kuvunjika kwa mfumo wa sasa wa dunia, akisema mataifa makubwa yanashindwa kuwajibika, na baadhi ya wadau waliounda mfumo huo sasa wamekuwa miongoni mwa wanaousambaratisha.

Pia alizungumzia kupungua kwa ufanisi wa taasisi zilizoundwa kudumisha amani, utulivu na kutatua migogoro ya kimataifa.

Alisema mabadiliko hayo yanaonekana pia katika sekta ya mawasiliano, akibainisha kuwa dunia imevuka “zama za mawasiliano” na kuingia katika kile alichokiita “wakati wa kuunda simulizi”.

“Katika wakati huu mpya, ushindani si tena kuhusu mawasiliano pekee, bali kuhusu namna uhalisia unavyoundwa, unavyotafsiriwa na hatimaye kukubalika mbele ya umma duniani,” alisema Duran.

Aliongeza kuwa ingawa ujumbe unaweza sasa kuwafikia watu duniani kote ndani ya sekunde chache, kasi hiyo pia inaleta hatari kama vile kuenea kwa taarifa potofu, upotoshaji na kufifia kwa mipaka kati ya ukweli na uongo.

Duran alisema migogoro si tena katika uwanja wa vita pekee, bali pia hupiganwa kupitia uundaji wa mtazamo na taarifa. Alionya kuwa video feki, maudhui yaliyobadilishwa na mitandao ya propaganda iliyopangwa zimekuwa sehemu muhimu ya migogoro ya kisasa.

“Kama Kurugenzi ya Mawasiliano, tunaona kuanzishwa kwa mfumo wa taarifa unaotegemea data sahihi, iliyohakikiwa na kuaminika kuwa kipaumbele chetu kikuu,” alisema.

Akisisitiza nafasi ya Uturuki katika masuala ya kimataifa, Duran alisema nchi hiyo imekuwa mpatanishi na mjenga amani katika migogoro kadhaa mikubwa, ikiwemo ile ya Iraq, Syria, eneo la Caucasus ya Kusini, Ukraine na Gaza.

Aliashiria kauli ya Rais Recep Tayyip Erdogan ya kwamba “dunia ni kubwa kuliko nchi tano” ni jibu la moja kwa moja kwa ukosefu wa usawa wa kimuundo katika mfumo wa kimataifa.

Jamii za Kiislamu kuunda taarifa zao

Burhanettin Duran pia alikosoa kutengwa kwa kihistoria kwa jamii za Kiislamu katika kuunda mfumo wa kimataifa, akibainisha kuwa zilikuwa zimeachwa nje ya michakato ya maamuzi wakati mfumo huo ulipowekwa miongo kadhaa iliyopita.

Akiashiria vitabu vilivyoandikwa na Edward Said, hasa ‘Orientalism na Covering Islam, akisema simulizi za Magharibi zimekuwa kwa muda mrefu zikichagia namna ulimwengu wa Kiislamu unavyoeleweka na kuwasilishwa.

Mkuu huyo wa Mawasiliano wa Uturuki alisema jamii za Kiislamu lazima zitoke katika hali ya kujilinda iliyowekwa na fikra za ki-Magharibi, na badala yake ziwe mbele na kuunda taarifa zao wenyewe katika mfumo mpya wa kimataifa unaoibuka.

“Mabadiliko ya leo hayaji tu na hatari tu, bali pia fursa,” alisema.

“Tunahitaji kurudisha maadili yetu ndani ya mfumo na kushinda mitazamo ya kujilinda inayochochewa na chuki dhidi ya Uislamu na mtazamo unaotawaliwa na fikra za Magharibi.”

Duran alitoa mfano wa nafasi ya makampuni ya teknolojia, makundi ya ushawishi, mitandao ya ujasusi na majukwaa ya kidijitali yasiyo na uwajibikaji wa moja kwa moja katika kuunda simulizi za dunia, akisema vinaathiri ni migogoro ipi inayopewa uzito na ni sauti za nani zinazosikika.

Wakati huohuo, alisema mazingira hayo pia yanatoa fursa kwa jamii za Kiislamu kuunda upya na kueleza simulizi zao wenyewe.

“Ikiwa hatutaweza kusimulia hadithi yetu wenyewe, wengine wataendelea kutusimulia,” alisema.

“Na ikiwa wengine wataisimulia hadithi yetu, wataamua nafasi yetu duniani.”

Alitoa wito wa ushirikiano imara kati ya serikali, mashirika ya kiraia, wasomi, wanahabari na wasanii, pamoja na uwekezaji zaidi katika ujuzi wa kidijitali na taasisi za kupambana na taarifa za upotoshaji.

Duran alieleza matumaini yake kwamba mazungumzo na ushirikiano uliotokana na jukwaa hilo utaimarisha umoja katika dunia ya Kiislamu na kuchangia kwa manufaa katika jamii ya kimataifa kwa ujumla.

CHANZO:TRT World