Mchungaji Mackenzie wa Shakahola matatani tena kwa kusababisha vifo vingine 52

Mackenzie alijipatia umaarufu kwa kuwahubiria waumini wake, washinde njaa, na baada ya kufa wakutane na Yesu.

By
Mchungaji Paul Mackenzie akiwa na watuhumiwa wenzake mahakamani./Picha:@ODPP_KE

Kiongozi wa dhehebu la njaa nchini Kenya, mchungaji Paul Mackenzie, siku ya Jumatano amesomewa shitaka la kusababisha vifo vingine 52, kupitia mahubiri yake.

Mackenzie, ambaye aligonga vichwa vya habari kufuatia dhehebu lake ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya waumini 400 nchini Kenya mwaka 2023, maarufu kama "Mauaji ya Msitu wa Shakahola", amekana madai hayo kufuatia mashitaka hayo, huku akiendelea kubakia rumande.

Hata hivyo, mwaka jana, miili zaidi iligundulika katika eneo la kijiji cha Binzaro, kilichopo kilomita 30 kutoka msitu wa Shakahola, pembezoni mwa Bahari ya Hindi, ikiashiria kwamba, bado dhehebu hilo lilikuwa likiendelea na ibada zake, hata baada ya kukamatwa kwa Mackenzie.

Kupitia taarifa yake iliyowekwa kwenye ukurasa wa X, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka nchini Kenya, ilisema kuwa imemshitaki Mackenzie na wenzake kwa kosa la kufanikisha vitendo vya kigaidi, kutokana na vifo vya watu wa 52, katika eneo la Kwa Binzaro, Kaunti ya Kilifi.

Washitakiwa hao walikana makosa hayo, huku kesi hiyo ikipangwa kusikilizwa tena Machi 4, mwaka huu.

"Wanatuhumiwa kwa kueneza imani hii ya kikatili ambayo imefanikisha vitendo vya kigaidi,” ilisema ofisi hiyo.