FIFA imejibu madai ya rais wa Shirikisho la Soka la Morocco kuwa taifa lake ndilo litakuwa mwenyeji wa mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2030, ikisema uamuzi huo bado haujafikiwa.
Morocco ni wenyeji wenza wa mashindano hayo ya 2030 pamoja na Hispania na Ureno. Hii itakuwa mara ya pili kwa nchi ya Afrika kuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Dunia, baada ya Afrika Kusini 2010.
Fouzi Lekjaa, mkuu wa Shirikisho la Soka la Morocco, inasemekana aliwaambia watu katika mkutano wa siasa siku ya Alhamisi kuwa taifa lake limepata nafasi za kuwa mwenyeji wa mechi ya fainali.
"Fainali ya Kombe la Dunia itachezwa katika mji wa Benslimane. Ukitaka usitake, na kama mtu yoyote anataka kupinga hilo, waendelee kupinga," Lekjaa alisema, kulingana na tafsiri ya shirika la habari la Associated Press. "Mji wa Benslimane, uwanja wa Hassan II ndiyo mwenyeji, na natumai kuwa Morocco itakuwa kwenye fainali hizo."
FIFA imeviambia vyombo kadhaa vya habari kuwa nchi ambayo fainali itachezwa itaamuliwa "katika muda muafaka."
Uwanja wenyewe, ambao rasmi unajulikana kama Mfalme Hassan II, bado unajengwa na hauko mbali na jiji la Casablanca, utakuwa na nafasi ya mashabiki 115,000.
FIFA imewahi kukanusha taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza kuwa rais Gianni Infantino, aliwaahidi Morocco fainali ili na yeye apate kuungwa mkono kisiasa wakati akitetea nafasi yake mwakani.


















