Uturuki yapinga hatua ya Israel kuhusu Somaliland, yaahidi kuimarisha ushirikiano na Somalia
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameitaja hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland kuwa “haikubaliki,” huku Uturuki ikiahidi kuendelea kuunga mkono Somalia katika masuala ya uchimbaji wa rasilimali, ulinzi, na diplomasia.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani hatua ya Israel wa kuitambua Somaliland kama taifa huru, akisema kuwa hatua hiyo si halali na ni changamoto ya moja kwa moja kwa uhuru wa mipaka ya Somalia.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Istanbul siku ya Jumanne pamoja na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Erdogan alisema Ankara inaunga mkono kwa dhati umoja na uhuru wa Somalia, akisisitiza kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya kiusalama nchini humo hayapaswi kudhoofishwa na “vitendo vya hujuma” kutoka kwa wahusika wanaopinga kupona kwa Somalia.
“Katika mchakato huu wote, tutaendelea kuwa thabiti katika kuunga mkono uhuru wa mipaka ya Somalia na umoja wake wa kisiasa, na tutaendelea kusimama pamoja na wananchi wa Somalia,” alisema.
Erdogan pia alisisitiza kuongezeka kwa ushirikiano wa kiuchumi na kimkakati wa Uturuki na Mogadishu, akitangaza mipango ya kuanza shughuli za uchimbaji mwaka 2026.
Alisema juhudi hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa wananchi wa Somalia, na akaeleza kuwa Uturuki imeongeza meli mbili mpya za uchimbaji wa raslimali katika bahari kuu kwenye safu zake za nishati.
Msaada wa Uturuki kwa Somalia
“Kwa Somalia, ambayo inaendelea kukabiliwa na vitisho dhidi ya uhuru wa mipaka ya eneo lake na uhuru wake, msaada wa Uturuki na wananchi wa Uturuki umeonekana wazi,” alisema Mohamud, akiishukuru Uturuki kwa msaada wake wa kisiasa, kiusalama, na kiuchumi.
Rais Mohamud pia alimkosoa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akielezea kutambuliwa kwa Somaliland na Israel kuwa ni hatua ya kichokozi na isiyokubalika inayokiuka uhuru wa Somalia.
Israel ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa imetambua Somaliland kama taifa huru lenye mamlaka kamili.
Somaliland imekuwa ikitenda kama eneo lenye uhuru tangu ilipotangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991, ikiwa na mifumo yake ya utawala, kisiasa, na kiusalama. Hata hivyo, imeshindwa kupata kutambuliwa rasmi kimataifa, huku serikali ya Somalia ikiendelea kulitambua eneo hilo kama sehemu muhimu ya eneo lake.
Somalia imekuwa ikikataa mara kwa mara mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Somaliland na serikali za kigeni, ikionya kuwa hatua kama hizo ni ukiukwaji wa umoja wa Somalia na sheria za kimataifa.
Mapokezi rasmi kwa Mohamud
Mapema siku ya Jumanne, Erdogan alimkaribisha Mohamud kwa sherehe rasmi katika Ikulu ya Rais ya Dolmabahce mjini Istanbul.
Viongozi hao wawili walifanya mkutano wa faragha kabla ya kuongoza kikao kikubwa cha wajumbe wa pande zote mbili.
Upande wa Uturuki uliwakilishwa na maafisa wakuu, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan, Waziri wa Nishati na Maliasili Alparslan Bayraktar, Waziri wa Ulinzi wa Taifa Yasar Guler, na Waziri wa Viwanda na Teknolojia Mehmet Fatih Kacir, pamoja na viongozi wakuu wa ujasusi, mawasiliano, na sekta ya viwanda vya ulinzi.