Afghanistan yafanya ‘mashambulizi ya kulipiza kisasi’ dhidi ya Pakistan
Jeshi la Pakistan lilifanya mashambulizi kando ya mpaka na Afghanistan, likisema limewaua angalau magaidi 70.
Msemaji wa Taliban nchini Afghanistan amesema walifanya “mashambulizi makali” dhidi ya Pakistan, siku chache baada ya Pakistan kushambulia “magaidi” nchini humo.
“Ili kulipiza mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Pakistan huko Nangarhar na Paktia, vikosi vya mpakani katika ukanda wa mashariki vilianzisha mashambulizi makali dhidi ya Pakistan,” Wahidullah Mohammadi, msemaji wa jeshi katika mashariki mwa Afghanistan, alisema katika ujumbe wa video siku ya Alhamisi.
Hadi sasa hakuna uthibitisho kutoka Pakistan wala taarifa kuhusu majeruhi.
Pakistan ilisema mashambulizi yake ya anga mwishoni mwa wiki yalilenga kambi za magaidi wa Tehrik-i-Taliban Pakistan (TTP) na Daesh mashariki mwa Afghanistan, huku vyanzo vya usalama vikieleza kuwa idadi ya magaidi waliouawa ilifikia 70.
Misheni ya Msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan ulisema umepokea “taarifa za kuaminika” kwamba angalau raia 13 waliuawa na saba kujeruhiwa huko Nangarhar.
Pakistan imeishutumu nchi jirani ya Afghanistan kwa kuwahifadhi magaidi wa TTP na kuwa chanzo cha kuongezeka kwa mashambulizi ya kuvuka mpaka, madai ambayo Afghanistan imeyakanusha.
Serikali ya Pakistan imeitaka serikali ya Afghanistan kuvunja maficho yanayodaiwa kuwa ya kundi la kigaidi la TTP ndani ya Afghanistan.
Kulingana na maafisa wa jeshi la Pakistan, zaidi ya watu 500, wakiwemo wanajeshi zaidi ya 311, waliuawa katika mashambulizi — mengi yakitekelezwa na TTP — mwaka uliopita.
Mnamo Oktoba, Pakistan pia ilifanya mashambulizi ndani ya Afghanistan kulenga maficho ya magaidi.