Uturuki yaahidi msaada zaidi kwa Sudan

Uturuki inalenga kuwasaidia watu wa Sudan na mamlaka za nchini humo katika kushughulikia matatizo ya watu.

By
Onal anasema wamepeleka mahema 30,000 nchini Sudna kwa meli tatu Disemba iliopita. / AA

Balozi wa Uturuki nchini Marekani amesisitiza msimamo wa Uturuki kuunga mkono kwa dhati umoja wa Sudan, mshikamano wao, na uhuru wa mipaka yake siku ya Jumanne, akiunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa kumaliza mzozo huo.

“Uturuki inasisitiza msimamo wake wa kuunga mkono kwa dhati umoja wa Sudan, mshikamano, na uhuru wa mioaka yake, ambayo tunaona ni muhimu kwa usalama wa Sudan na kanda nzima,” Sedat Onal alisema katika hafla moja kuhusu uchangishaji fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Sudan katika Taasisi ya Amani ya Marekani jijini Washington, DC.

“Tunaamini kuwa njia thabiti ya kumaliza mzozo huu ni kutumia majadiliano na diplomasia. Tunaunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa zenye lengo la kumaliza mgogoro,” Onal alisema.

Hafla hiyo iliratibiwa na Massad Boulos, mshauri mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu masuala ya Arabuni na Afrika, na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya misaada kwa watu na Mratibu wa Dharura (OCHA) Tom Fletcher pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Marekani na wanadiplomasia kutoka Saudi Arabia, UAE, Misri, Uingereza, Ufaransa na nchi zingine.

Kukabiliana na mahitaji kwa watu

Onal anasema lengo pekee la Uturuki katika mazingira ya sasa ni kusaidia watu wa Sudan na kusaidia mamlaka za Sudan katika kukabiliana na mahitaji ya watu wa Sudan.

Alieleza kuwa Uturuki ilikuwa moja ya nchi za kwanza kusaidia watu wa Sudan tangu mapigano yalipoanza.

Sudan imekuwa katika vita kati ya jeshi na wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) tangu Aprili 2023, kusababisha mauaji ya maelfu ya watu na mamilioni wengine kubaki bila makazi.

Mwaka uliopita tarehe 26 Oktoba, RSF ilichukua udhibiti wa Al Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, na kuhusika na mauaji ya kikatili dhidi ya raia, kulingana na mashirikia ya kitaifa na kimataifa, huku kukiwa na onyo kuwa mashambulizi hayo yatasababisha kugawanywa kwa nchi.

Msaada wa Uturuki

Onal anasema kuwa mahema 30,000 yalipelekwa Sudan kupitia meli tatu Disemba iliopita kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) kufuatia matukio “ya kikatili” huko Al Fasher.

“Shirika la Hilali Nyekundu la Uturuki na Mashirika kadhaa yasiyokuwa ya Kiserikali ya Uturuki yanaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa watu kuanzia chakula na makazi na bidhaa zingine kwa watu wanaohitaji kwenye maeneo kadhaa nchini Sudan,” alisema, akieleza kuwa Uturuki itaendelea kutoa misaada “katika wiki zijazo.”

Mkutano huo wa wafadhili wa Washington unakuja huku Marekani ikitaka kuchangisha hadi dola bilioni 1.5 kwa Sudan juhudi zikiendelea za kutafuta makubaliano ya kutoa misaada kwa watu kabla ya mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhan, ambao unaanza mwezi huu.