Kwa nini Afrika Mashariki haikuwa na kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta kabla ya mradi wa Dangote wa Lamu?
Kenya ilikuwa na kiwanda cha kusafisha mafuta mjini Mombasa, kilichoanzishwa mwaka 1960, na kitengo chake cha kwanza cha uchakataji kilianza kufanya kazi mwaka 1963.
Kitengo cha pili kiliongezwa mwaka 1974, na kuongeza uwezo wa kiwanda hicho kufikia takriban tani milioni 4 za mafuta ghafi kwa mwaka.
Katika kipindi chake cha mafanikio makubwa, kiwanda hicho kilikidhi takriban asilimia 40 ya mahitaji ya bidhaa za mafuta nchini Kenya na pia kilihudumia masoko katika eneo pana la Afrika Mashariki.
Hata hivyo, uchakataji wa mafuta ghafi ulisimama mwaka 2013, huku serikali ya Kenya ikibainisha changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa nishati ya umeme ya uhakika, uchakavu wa mitambo, upungufu wa maji na ugumu wa kukidhi viwango vipya vya ubora wa mafuta.
Kwa sasa, kituo hicho kinatumika kama sehemu ya kuhifadhia mafuta chini ya kampuni ya Kenya Petroleum Refineries Limited (KPRL).
Kiwanda cha mafuta Tanzania
Tanzania nayo ilikuwa na kiwanda cha kusafisha mafuta.
Kiwanda cha TIPER nchini Tanzania kilianzishwa katika miaka ya 1960 kama ubia kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya AGIP ya Italia.
Kilikuwa na uwezo wa kuchakata takriban tani 600,000 za mafuta ghafi kwa mwaka — sawa na mapipa takriban 12,000 kwa siku.
Hata hivyo, uendeshaji wa kiwanda hicho ulianza kutokuwa na tija kiuchumi. Hivyo, Tanzania iliamua kuanza kuagiza bidhaa za mafuta zilizokwisha kusafishwa.
Kufikia mwaka 1999–2000, TIPER ilikuwa imeacha kufanya kazi kama kiwanda cha kusafisha mafuta na kubadilishwa kuwa kituo cha kuhifadhia mafuta.
Changamoto ya kuanzisha na kuendesha viwanda vya kusafisha mafuta
Hivyo, ni kwa nini baadhi ya nchi zinakabiliwa na changamoto ya kuanzisha na kuendesha viwanda vya kusafisha mafuta?
Changamoto kubwa zaidi inakuwa kwenye gharama.
Kwa mfano, kiwanda cha kusafisha mafuta kilichopangwa kujengwa Hoima, nchini Uganda, kitakuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 60,000 ya mafuta ghafi kwa siku na kitahitaji uwekezaji wa takriban Dola bilioni 4.
Kwa kulinganisha, kiwanda kinachopendekezwa cha Dangote huko Lamu kimepangwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 kwa siku, huku gharama yake ikikadiriwa kuwa kati ya Dola bilioni 15 na 16.
Upatikanaji wa mafuta ghafi
Kisha kuna suala la upatikanaji wa mafuta ghafi.
Uganda ina takriban mapipa bilioni 1.4 ya mafuta yanayoweza kuchimbwa, lakini mafuta hayo yanapatikana maeneo ya ndani ya nchi. Kuyasafirisha kunahitaji miundombinu mikubwa, ikiwemo Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilomita 1,443 linaloelekea Tanga, pwani ya Tanzania.
Kenya pia kwa sasa haizalishi mafuta ghafi ya kutosha kuendesha kiwanda chenye ukubwa kama ule wa mradi unaopendekezwa wa Lamu.
Mafuta yatahitajika kupatikana kutoka Uganda, Sudan Kusini na Kenya, lakini kila chaguo lina changamoto zake ikiwemo za usafirishaji.
Upatikanaji wa soko
Tatizo jingine ni ukubwa wa soko.
Kiwanda cha kusafisha mafuta kinahitaji kufanya kazi kwa uwezo mkubwa ili kufidia gharama zake kubwa za ujenzi.
Kihistoria, masoko ya nchi moja-moja za Afrika Mashariki yamekuwa madogo mno kuhalalisha ujenzi wa viwanda vikubwa sana, jambo linalofanya soko la kikanda kuwa muhimu zaidi.
Hivyo, mradi wa Dangote wa Lamu unawakilisha mbinu tofauti: kiwanda kikubwa kitakachohudumia soko la kikanda badala ya kutegemea mahitaji ya nchi moja pekee.





















