| Swahili
ULIMWENGU
3 dk kusoma
Putin asema Urusi ni mshirika bora kwa Afrika kuliko nchi zenye historia ya ukoloni
Rais Vladimir Putin anaishutumu nchi za Magharibi kwa kuendelea kujaribu kunyonya rasilimali za bara la Afrika na kutumia madeni kama njia ya kukwamisha maendeleo yake.
Putin asema Urusi ni mshirika bora kwa Afrika kuliko nchi zenye historia ya ukoloni
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akiwa na viongozi wa Afrika katika mkutano kati ya Urusi na Afrika jijini Moscow. /

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, aliwaambia viongozi wa Afrika siku ya Jumatano kwamba Urusi ni mshirika bora zaidi kwa bara hilo. Alizishutumu nchi za Magharibi, ambazo alizitaja kuwa na mtazamo wa kikoloni, kwa kuendelea kujaribu kunyonya rasilimali za Afrika na kutumia madeni kuzuia maendeleo ya bara hilo.

Kiongozi huyo wa Urusi alikuwa akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Urusi na Afrika uliofanyika jijini Moscow. Mkutano huo wa siku mbili ulihudhuriwa na viongozi wa Afrika pamoja na wajumbe wa serikali kutoka nchi 48. Katika mkutano huo, Putin alipanga kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi 22 wa Afrika waliohudhuria, yakihusu masuala mbalimbali, yakiwemo biashara, usalama, mikataba ya silaha na usambazaji wa nafaka.

Mkutano huo, uliofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2019, ni sehemu ya juhudi za Urusi za kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi na nchi za bara la Afrika.

“Afrika inazidi kujidhihirisha kama mmoja wa wadau wakuu katika uchumi na siasa za dunia. Hata hivyo, kuibuka kwa mfumo wa dunia wenye mataifa kadhaa yenye nguvu na ushawishi; ni jambo lisilo rahisi. Kunakabiliwa na upinzani kutoka kwa nchi ambazo haziko tayari kukubali hali hii halisi; nchi zilizozoea kufikiri kwa mtazamo wa historia yao ya ukoloni na kujitajirisha kupita kiasi,” Putin aliwaambia walioshiriki mkutano huo. 

Putin pia alizungumzia kile alichokiita “juhudi za nchi za Magharibi” za kuwarudisha Waafrika katika hali ya kukwamisha maendeleo ya Afrika kupitia madeni. Alidai kuwa nchi hizo zinajaribu kuwalazimisha Waafrika kupokea fedha wanazozihitaji kwa masharti magumu yanayonufaisha wakopeshaji, hali ambayo, kwa mujibu wake, inakwamisha maendeleo ya muda mrefu ya bara hilo.

Kushirikishana utaalamu na teknolojia

Kwa upande mwingine, Putin alisema Urusi iko tayari kushirikiana na Afrika kwa kubadilishana utaalamu, ikiwemo teknolojia za kidijitali, na kuhamishia shughuli za uzalishaji katika nchi za Afrika badala ya kununua malighafi pekee.

“Biashara zetu hazijihusishi na unyonyaji wa rasilimali na raslimali watu kwa mtindo wa ukoloni mamboleo. Badala yake, zinapanua shughuli za uchakataji wa malighafi ndani ya nchi husika, hatua inayosaidia kutengeneza ajira na kuongeza mapato ya kodi,” alisema Putin.

Putin aliwaambia walioshiriki mkutano huo kwamba Urusi inaunga mkono kuongezwa kwa ushawishi wa Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia. Alisema pia kuwa nchi yake iko tayari kuanzisha miradi ya pamoja ya usafiri na miundombinu ya kilimo.

Aidha, alisema idadi kubwa zaidi ya wanfunzi kutoka afrika, takribani 40,000, wanasoma katika vyuo vikuu vya Urusi.

Putin aliongeza kuwa Urusi iko tayari kusambaza nafaka na mbolea kwa nchi nyingi zaidi za Afrika, zaidi ya nchi 40 ambazo tayari zinapokea bidhaa hizo kutoka Urusi.

Kwa mujibu wa Putin, Urusi ilikuwa imesambaza jumla ya tani milioni 13 za bidhaa za kilimo barani Afrika katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huo pekee.

CHANZO:AP