CAF yashtumu utovu wa nidhamu robo fainali AFCON 2025, yaanzisha uchunguzi
Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) linasema matukio katika mechi zote mbili yamewasilishwa kwa Kamati ya Nidhamu kwa uchunguzi kamili.
Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) limeshtumu vikali kile walichokitaja kuwa ‘‘tabia isiyokubalika” ya wachezaji na maafisa wakati wa mechi mbili za robo fainali kwenye AFCON 2025 nchini Morocco, na imeanzisha uchunguzi rasmi kuhusu matukio hayo.
Katika taarifa siku ya Jumatatu, CAF inasema imetathmini ripoti ya mechi na ushahidi wa video zikidhihirisha uwezekano wa utovu wa nidhamu wakati wa michuano ya robo fainali kati ya Cameroon na Morocco, na Algeria na Nigeria.
Nchi wenyeji Morocco ilishinda 3–2 dhidi ya Cameroon mechi ya robo fainali, iliyomalizika kwa uhasama.
Wachezaji kadhaa wa timu zote mbili walikabiliana uwanjani, huku maafisa wakiwatenganisha wakati timu zikitoka uwanjani.
Hisia kali baada ya mechi
Katika mechi nyingine ya robo fainali, Nigeria iliishinda Algeria 2–0, mechi ambayo Algeria ililalamika, ikidai kuwa matokeo yalichochewa na uamuzi mbaya, ikiwemo kilio cha penati cha Algeria ambacho hakikusikilizwa.
Hasira zilitokana na wachezaji na maafisa wa Algeria, na makabiliano yakazuka punde tu baada ya mechi. Maafisa wa usalama na waamuzi waliingilia kati kutuliza hali huku kukiwa na vuta nikuvute karibu na maeneo ya mabenchi ya ufundi.
Maafisa wa usalama walilazimika kumzunguka muamuzi Issa Sy na wasaidizi wake, Djibril Camara na Nouha Bangoura, wakati wakitoka uwanjani. Maafisa pia walipata tabu kuwatuliza baadhi ya wachezaji wa Algeria ambao walijaribu kufika karibu na walipo waamuzi.
CAF inasema matukio hayo kutoka kwa mechi zote mbili yamewasilishwa kwa Kamati ya Nidhamu kwa uchunguzi kamili, huku vikwazo zaidi vikitarajiwa iwapo wachezaji au maafisa binafsi watapatikana na hatia.
‘Utovu wa nidhamu’
“CAF inashtumu vikali utovu wa nidhamu wakati wa mechi hizo, hasa ulioelekezwa kwa maafisa wa mechi, waamuzi, au waandaaji wa michuano,” taarifa ilisema. “Tabia kama hizo haziendani na viwango vyetu vya kitaalamu kama inavyotarajiwa katika mashindano ya CAF.”
Shirikisho hilo la soka la Afrika pia limethibitisha linafanyia tathmini video nyingine kuhusu waandishi wa habari, ambao walidaiwa kujuhusisha na vitendo visiokubalika kwenye eneo la mahojiano baada ya mechi za robo fainali.
CAF imesisitiza kuhusu suala la nidhamu na heshima wakati wa mashindano, ikisema kuwa hatua kali zitachukuliwa kulinda hadhi ya AFCON.