| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Ofisi ya Rais Tanzania yatetea haki ya uhamisho kwa watumishi wa umma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesisitiza umuhimu wa kuboresha usimamizi wa watumishi wa umma nchini.
Ofisi ya Rais Tanzania yatetea haki ya uhamisho kwa watumishi wa umma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais amesisitiza haki ya uhamisho kwa watumishi wa umma. / TRT Afrika Swahili

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesisitiza umuhimu wa kuboresha usimamizi wa watumishi wa umma nchini, huku akitahadharisha Wakuu wa Taasisi na Wakurugenzi kuacha kuzuia barua za uhamisho wa watumishi wa umma.

Amesema hatua ya kuzuia uhamisho ni kinyume cha taratibu za utumishi wa umma na inawanyima watumishi haki yao ya msingi, akibainisha kuwa mamlaka ya uhamisho iko chini ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mkomi ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuelekea kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu kutoka taasisi mbalimbali za serikali, kitakachofanyika Dodoma kuanzia Juni 1 hadi 3, 2026.

Amesema kikao hicho kitajadili kwa kina matumizi ya mifumo ya kidijitali ya e-Uhamisho, e-Watumishi na e-Utendaji, pamoja na changamoto na mafanikio katika usimamizi wa rasilimali watu, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utumishi wa umma kuelekea Dira ya Taifa 2050.