Israel lazima isitishe mara moja kukiuka makubaliano ya usitishaji vita Gaza: Uturuki

Uturuki pia imesema kuwa Ankara itaendelea kutoa msaada wa amani, ustawi, na usalama kwa matabaka yote ya wananchi wa Syria.

By
Uturuki inasema Israel lazima isitishe mara moja mashambulizi yanayokiuka makubaliano ya Gaza. / AA

Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki limesema kuwa Israel lazima isitishe mara moja mashambulizi yanayokiuka makubaliano ya usitishaji vita Gaza na itimize wajibu wake.

Baraza hilo limesema kuwa Uturuki iko tayari kuchukua majukumu katika mifumo itakayohakikisha utulivu Gaza na kuchangia jitihada za ujenzi upya. Katika taarifa iliotolewa Jumatano.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, aliongoza mkutano huo katika Ikulu ya Rais jijini Ankara.

Kulingana na makubaliano ya usitishaji vita yaliyoanza kutekelezwa Oktoba 10, mabasi 600 ya misaada yalipaswa kuingia Gaza kila siku. Hata hivyo, Israeli inaruhusu mabasi ya misaada yasiozidi 200 kuingia Gaza kwa siku.

Israel haijafuata makubaliano hayo, ikifanya mashambulizi karibu kila siku ambayo yamesababisha vifo vya angalau Wapalestina 342 tangu Oktoba 10.

Israel imewaua watu zaidi ya 70,000, wengi wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine zaidi ya 170,700 katika mashambulizi dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023.

Ankara itaendelea kutoa msaada wa amani, ustawi, na usalama kwa makundi yote ya wananchi wa Syria, Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki limesema.

Baraza hilo pia liliangazia hali ya hivi karibuni katika vita vya Urusi na Ukraine na kuthibitisha jitihada za Uturuki zinazoendelea pamoja na washirika wake wa kimataifa kuanzisha amani ya haki na ya kudumu.