China imeonya dhidi ya mzozo wa Mashariki ya Kati kuenea hadi Pembe ya Afrika, ikisema kuwa eneo hilo “halipaswi kamwe kuwa uwanja wa ushindani wa siasa za kijiografia.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Abdoulkader Houssein Omar, walikubaliana kuhusu kutoenea mzozo huo wakati wa mkutano wao uliofanyika Beijing, China, siku ya Jumanne.
Kwa mujibu wa Mao Ning, viongozi hao walieleza kuwa kuongezeka kwa mvutano katika Bahari ya Shamu kunatishia uchumi wa dunia, hususan shughuli za kiuchumi katika eneo hilo na unazidisha changamoto za kiusalama, zikiwemo uharamia na ugaidi.
Mao Ning alisema mawaziri hao wawili wamezitaka pande husika kuheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN), kuzingatia kanuni za kimataifa na kuepuka kuchochea zaidi mvutano huo. Alisisitiza kuwa mazungumzo na diplomasia vinapaswa kutumika kutafuta suluhisho la mzozo huo.
“Pembe ya Afrika haipaswi kamwe kuwa uwanja wa ushindani wa kisiasa na kijiografia, na mzozo wa Mashariki ya Kati haupaswi kuenea hadi Pembe ya Afrika,” alisema Mao.






















