Viwanja vya mpira vya Kenya na Uganda bado havijakuwa tayari kwa michuano ya AFCON 2027
Ripoti mpya ya Shirikisho la Soka Afrika, CAF, imesema kuwa hadi kufikia Februari 2026 viwanja vya michezo nchini Kenya na Uganda vilikuwa bado haviko tayari kuhodhi michuano.
Uganda imesema inajitahidi kurekebisha mapengo ambayo yamebainishwa na Shirikisho la Soka Afrika wakati ikijiandaa kuandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027 pamoja na Kenya na Tanzania.
Ripoti mpya ya Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, inafichua kuwa kufikia Februari 2026, hakuna uwanja wowote kati ya viwanja vinne vilivyopendekezwa nchini Uganda unaokidhi viwango kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
CAF ilifanya uchunguzi wa viwanja na vifaa vya michezo katika nchi wenyeji Februari 2026 kama sehemu ya ukaguzi na udhibiti wa ubora kuelekea AFCON 2027.
"Ni kweli kwamba CAF, ripoti yao, ilitaja mapungufu machache, kuna mapungufu katika uwanja wa Hoima ambayo yamesababishwa na mkandarasi," Peter Ogwang, Waziri wa Nchi, Elimu na Michezo alifafanua kupitia mtandao wa X.
Mapendekezo ya CAF ni pamoja na kubadilishia maeneo ya wachezaji kubadilishia nguo, maeneo ya vyombo vya habari, vifaa vya watazamaji, na kurekebishwa kwa paa.
"Kwa kweli, tangu wakati huo mkandarasi amefanya mikutano kadhaa na sisi na anatuhakikishia kuwa masuala yaliyoibuliwa yanashughulikiwa kwa kujadili ili kukidhi matakwa na viwango vya CAF kabla ya ukaguzi ujao wa Agosti mwaka huu," alifafanua.
Amesema mahitaji mengine ya CAF yanayohusisha Uwanja vya Ndege, barabara na hoteli, viko nje ya sekta ya Michezo, yameelekezwa kwa Wizara husika na imeripotiwa kuwa Baraza la Mawaziri limekubali kutatua changamoto hizo.
Mapungufu katika vifaa vya michezo Kenya
Ripoti ya CAF pia inaangazia mabadiliko makubwa yanayohitaji kufanywa katika viwanja vitatu vya Kenya.
Ripoti hiyo inaangazia kwamba mpango wa miundombinu ya Kenya uko katika hatua ya ujenzi, uboreshaji, na uundaji upya wa uendeshaji, na mapungufu makubwa katika maeneo muhimu.
"Wakati Kenya inanufaika kutokana na mazingira thabiti ya jiji la Nairobi, mpango wa utoaji unasalia wazi kutokana na ukubwa wa uboreshaji wa kimuundo unaohitajika, utegemezi wa ujenzi mpya na utayari usio sawa wa miundombinu ya mafunzo," ripoti ya CAF ya Februari ilibainisha kwa sehemu.
CAF ilipendekeza uthibitisho wa mwisho wa mzunguko wa watazamaji na mipango ya kutenganisha, uthibitisho wa eneo la Kituo cha Uendeshaji cha Ukumbi, na ujumuishaji unaofaa wa kanda za timu, maafisa na waandishi wa habari.
Masuala mengine kama vile taa, nishati mbadala, na miundombinu ya usalama pia bado yanahitaji kushughulikiwa.
Waziri wa Michezo wa Kenya Salim Mvurya amelihakikishia taifa kwamba maandalizi yanaendelea vizuri, akibainisha kuwa serikali inajitahidi kutimiza majukumu ya kifedha na miundombinu, ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya kuwa mwenyeji ya Dola milioni 30M (Ksh 3.9 bilioni) kabla ya Machi 30.