Je, Uchaguzi wa Sudan Kusini utaleta amani au migogoro?
SIASA
6 dk kusoma
Je, Uchaguzi wa Sudan Kusini utaleta amani au migogoro?Serikali inasema Uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 2026 unaweza kufungua njia ya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayohitajika kwa muda mrefu.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu utafanyika Disemba 2026

Katika eneo mbali la jimbo la Magharibi mwa Equatoria, nchini Sudan Kusini, Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo kinaandaa mazingira salama kwa jamii ya kutatua migogoro, kuimarisha maridhiano na kuandaa mipango ya pamoja ya kufanikisha amani ya kudumu.

Wakazi wengi wa eneo hili hawajashuhudia kuwepo kwa amani ya kudumu tangu kuzuka kwa mzozo kati ya serikali ya Rais Salva Kiir na vikosi vya upinzani mwaka 2013.

Wanatamani kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu, ikiwemo kulima, watoto wao kwenda shule, na kujenga maisha bora.

Wanaamini kuwa amani ya kudumu huanza kwa kushughulikia malalamiko kwa uwazi kabla hayajageuka kuwa migogoro.

“Kinachonifurahisha ni kile ninachokifanya kwa ajili ya jamii yangu. Kunapokuwa na mzozo kati ya mwanamume na mwanamke, mimi huwa mwepesi kwenda kuutatua na kurejesha amani ili tuishi kwa maelewano,” Lois Wilson, Mkazi wa Bazungua anaelezea viongoiz wa Umoja wa mtaifa ambao wanasaidi jamii hii kujikimu.

Katika maeneo mengine ya jimbo hilo, barabara mbovu na ukosefu wa usalama vimefanya upatikanaji wa bidhaa muhimu kuwa mgumu zaidi.

“Hali ya usalama barabarani inatuathiri sana kwa sababu barabara hiyo ndiyo njia yetu kuu ya mawasiliano na usafirishaji, “ John Aurupai Anash, Chifu wa Kaunti ya Ibba anasema.

“Mwezi Mei, baadhi ya vijana wetu walisafiri kwenda Juba kununua bidhaa. Walipokuwa wakirejea, walitekwa nyara, na hadi sasa hawajapatikana.”

Changamoto ya maisha Sudan Kusini

Hii ndiyo hali ya maisha ya wengi katika nchi hii changa barani Afrika.

Takriban watu milioni mbili waliolazimika kuyahama makazi yao ndani ya nchi bado hawajui lini watarudi nyumbani, huku wengine takriban milioni 2.5 wanaendelea kuwa wakimbizi katika nchi za nje.

Serikali inasema Uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 2026 unaweza kufungua njia ya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayohitajika kwa muda mrefu.

Cecilia Adout Majok Adeng, Waziri wa Mambo ya Nje wa Muda aliambi mkutano wa Umoja wa Afrika Septemba 2026,

“Maono ya Rais Kiir ni kuweka mazingira yatakayowezesha dunia kuwaona tena wananchi wa Sudan Kusini jinsi walivyo hasa: watu wenye ustahimilivu ambao walipigania uhuru, walipiga kura kwa amani ili kupata uhuru na wanaoendelea kutamani amani, utu, demokrasia na ustawi.”

Hata hivyo, ikiwa imesalia miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu, maandalizi muhimu bado hayajakamilika.

Sudan Kusini bado haina daftari la mpiga kura lililokamilika.

Mahitaji ya uchaguzi hayajashughulikiwa

Ingawa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeandaa vifaa vya usajili, haikuwa imethibitishwa kuwa zoezi la usajili wa wapiga kura limeanza.

Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Afrika za Septemba 2026, uchaguzi huo unahitaji takriban Dola milioni 250 za Marekani. Serikali ilikuwa tayari imetoa karibu Dola milioni 27, hivyo kuacha pengo la ufadhili la takriban Dola milioni 223.

Mnamo Oktoba 2026, Rais Kiir aliitembelea Kenya na Afrika Kusini na kufanya mazungumzo na viongozi wenzake kuhusu uwezekano wa kupata msaada wa kifedha kwa ajili ya kuendesha zoezi la Uchaguzi, ukiwemo usaidizi wa kiufundi na vifaa vya uchaguzi.

Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini alisema katika mkutano wa Umoja wa Afrika uliojadili Uchzguzi wa sudan kusini Oktoba 2026,

“Tunafahamu kuwa uchaguzi pekee hauwezi kuhakikisha amani na demokrasia. Uchaguzi wa kuaminika unapaswa kutanguliwa na kuambatana na mchakato wa kisiasa wa kweli na jumuishi, ukiungwa mkono na mipango ya usalama pamoja na ulinzi wa maafisa wa uchaguzi, mchakato wa uchaguzi na raia.”

Tangu kupata uhuru mwaka 2011, Sudan Kusini imeahirisha tarehe ya Uchaguzi Mkuu kwa takriban mara tano.

Mivutano ya kisiasa

Hii imechangiwa na migogoro na mivutano ya kisiasa inayoibuka mara kwa mara.

Tarehe ya mwisho ya kuahirishwa kwa Uchaguzi huo, ilikuwa ni mwaka 2024, ambapo Uchaguzi ulisogezwa hadi Disemba 2026.

Nchi hiyo bado inaongozwa na Mkataba wa Makubaliano ya Kutatua Mgogoro wa Sudan Kusini, uliotiwa saini tarehe 12 Septemba 2018 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkataba huo ulipanga kipindi cha mpito cha miezi 36, yaani miaka mitatu, kitakachoongoza kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Hata hivyo, ucheleweshaji wa utekelezaji na kuahirishwa kwa uchaguzi mara kwa mara kumeongeza muda wa kipindi hicho cha mpito.

Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa kipindi hicho kinapaswa kumalizika Februari 2027.

Edmund Yakani, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kiraia cha CEPO alisema,

“Wakati umefika. Wananchi wamesema tupe nafasi ya kuamua viongozi wetu ni nani. Lakini tupe nafasi hiyo pale ambapo mazingira yanayofaa yatakuwa yameandaliwa na kutimizwa.”

Hata hivyo, mabadiliko makubwa ya kisiasa yaliyotokea miezi michache kabla ya uchaguzi yameongeza hali ya wasiwasi.

Mabadiliko ya kisiasa

22 Septemba 2026, Rais Kiir alivunja serikali ya mpito iliyoundwa chini ya mkataba wa amani wa mwaka 2018.

Aliwaondoa makamu wa rais wote watano, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya jinai.

Bunge la kitaifa, serikali za majimbo na mabunge yake, pamoja na mamlaka za kiutawala katika maeneo matatu, pia zilivunjwa. Baraza la Mawaziri lilifutwa na nafasi zake kujazwa na maafisa walioteuliwa kuwa mawaziri wa muda.

“Ninataka nyote muwe nami. Mwanzo mpya unamaanisha kwamba ninyi kama mawaziri wangu lazima mchukue hatua haraka, kama ninavyowaelekeza, ” Rais Salva Kiir, aliwaaambia viongozi hao wa muda walipokuwa wakiapishwa.

Kiir anaendelea kuwa Rais na atatekeleza mamlaka ya serikali hadi pale Rais atakayechaguliwa atakapochukua madaraka.

Mabadiliko hayo yameibua wasiwasi kuhusu makubaliano ya kisiasa na mustakabali wa mfumo wa kugawana madaraka ulioanzishwa na mkataba wa amani.

Marekebisho ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pia yaliondoa sharti la kukamilisha katiba ya kudumu na kufanya sensa ya kitaifa kabla ya Uchaguzi.

Ushiriki wa upinzani katika uchaguzi

Serikali inasema hatua hiyo inaondoa vikwazo kwa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu.

Hata hivyo, makundi ya upinzani na wachambuzi wanaonya kuhusu kuongezeka kwa madaraka katika Ofisi ya Rais.

Gabriel Bol Deng, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alisema,

“Kwa hiyo, ninatoa wito kwa wanasiasa wetu na vyama vyetu vya kisiasa kubadilisha mawazo yao ya kisiasa kuwa kura kwenye karatasi za kupigia kura, badala ya risasi. Ni jukumu la kila mwanasiasa, kila chama cha kisiasa na kila raia kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unakuwa wa amani.”

Ushiriki wa upinzani ni changamoto nyingine.

Machar, aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, anakabiliwa na kesi ya jinai, hali inayoibua maswali kuhusu iwapo upinzani utaweza kushiriki kwa uhuru katika uchaguzi.

Hali ya usalama haijaimarika

Hali ya usalama pia bado ni tete.

Mapigano yanayohusisha vikosi vya serikali na vile vinavyohusishwa na upinzani, pamoja na ghasia za kijamii katika baadhi ya maeneo ya nchi, yanaendelea kutishia utulivu.

Mchakato wa kuunganisha na kupeleka kazini vikosi vya kijeshi vya pande hasimu pia haujakamilika, jambo linalozua mashaka kuhusu uwezo wa serikali kuhakikisha uchaguzi wa amani.

Licha ya changamoto hizi, serikali imesisitiza kuwa itaendelea na Uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Disemba 2026, ikiutaja kuwa fursa ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na utulivu ambao wananchi wameutafuta tangu uhuru.

Cecilia Adout Majok Adeng, Waziri wa Mambo ya Nje wa Muda aliihakikishia dunia katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, Septemba 2026,

“Sudan Kusini bado imejizatiti katika safari ndefu ya kubadilisha dhabihu zilizotolewa katika ukombozi kuwa amani, utu, maendeleo na mustakabali wa kidemokrasia ambao wananchi wa Sudan Kusini wameusubiri kwa vizazi vingi. Hiyo ndiyo ahadi ya uhuru.”

Hii ni ahadi ambayo wananchi wengi ambao wamekuwa wakitafuta njia zao wenyewe za kujilinda wanasubiri kuona iwapo matumaini hayo yatatimia.

CHANZO:TRT Swahili