| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Urusi na China zaimarisha ushirikiano kwa kusaini mikataba 20 ikiwemo ya uchumi, nishati na biashara
Urusi na China zinaongeza kasi ya juhudi za kupanua matumizi ya sarafu zao za kitaifa katika malipo ya biashara, huku zikilenga kulinda uchumi wao dhidi ya mabadiliko ya soko la dunia na kupunguza utegemezi kwa Dola ya Marekani.
Urusi na China zaimarisha ushirikiano kwa kusaini mikataba 20 ikiwemo ya uchumi, nishati na biashara
Rais wa Urusi alielezea ushirikiano wa Urusi na China kama jambo linaloleta utulivu katika masuala ya kimataifa. / / Reuters

Urusi na China zilisaini mikataba 20 ikiwemo ya uchumi, nishati, usafiri na ushirikiano wa kimataifa baada ya mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China Xi Jinping mjini Beijing siku ya Jumatano.

Viongozi hao wawili walipitisha taarifa ya pamoja kuhusu kuimarisha zaidi ushirikiano na kuendeleza mahusiano kati ya Urusi na China, pamoja na tamko la pamoja kuhusu kuunda dunia yenye nguvu nyingi (multipolar world) na aina mpya ya mahusiano ya kimataifa.

Urusi na China zimejenga mfumo thabiti wa biashara ya pande mbili ambao unalindwa dhidi ya shinikizo la nje na misukosuko ya masoko ya dunia, Putin alisema katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na Xi.

Alieleza kuwa kufanya biashara kwa kutumia sarafu ya Ruble na Ruan kunasaidia kulinda ushirikiano wa kiuchumi dhidi ya “ushawishi wa nje” na kuhakikisha uimara wa mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

“Hatua zilizoratibiwa zilizochukuliwa na Urusi na China za kutumia sarafu zaou za kitaifa zimekuwa na umuhimu mkubwa. Matokeo yake, karibu shughuli zote za uagizaji na usafirishaji bidhaa kati ya Urusi na China zitafanyika kwa Ruble na Yuan,” alisema.

Putin pia alisema kuwa Urusi iko tayari kuendelea kusambaza mafuta na gesi kwa China bila kukatizwa, na kwamba shirika la nyuklia la Urusi, Rosatom, linakamilisha ujenzi wa vitengo vipya vya kuzalisha umeme katika mitambo ya nyuklia nchini China kama sehemu ya ushirikiano mpana wa nishati kati ya nchi hizo mbili.

Rais huyo wa Urusi pia alielezea ushirikiano wa Urusi na China kama sababu ya kuleta utulivu katika masuala ya kimataifa.

Putin aliongeza kwa kusema kuwa mfumo wa kutohitaji visa kati ya nchi hizo mbili umeonyesha matokeo mazuri, jambo ambalo limeongeza utalii na mawasiliano kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

“Mwaka 2025, zaidi ya Warusi milioni 2 walizuru China. Zaidi ya raia milioni 1 wa China walitembelea Urusi,” alisema.

CHANZO:AA