Kenya imemteua mgombea katika uchaguzi wa majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
ICC ni mahakama ya kimataifa iliyoko mjini The Hague, Uholanzi, ambayo inasimamia kesi za watu binafsi wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na uchochezi.
Rais wa Kenya William Ruto amemteua Jaji wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, Njoki Ndung’u, kuwania nafasi ya jaji wa ICC.
Uchaguzi wa majaji wa ICC umeratibiwa kufanyika katika kikao cha ishirini na tano cha Bunge la Nchi Wanachama, kitakachofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, kuanzia tarehe 7 hadi 17 Disemba 2026.
"Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu watachaguliwa miongoni mwa watu kwa kuzingatia maadili yao, wasiokuwa na upendeleo na waadilifu ikiwa ni baadhi ya sifa zinazohitajika katika Mataifa yao kwa ajili ya kuteuliwa kwa wadhifa huo wa juu zaidi wa mahakama," ICC inasema kwenye tovuti yake.
Bunge la Nchi Wanachama litachagua majaji sita.
Jaji Njoki Ndung'u, ni mgombea wa nne kutoka Afrika ikiwa wengine waliopendekeza wagombea ni kutoka mataifa ya Tanzania, Uganda na Ghana.
Hadi sasa nchi nane zina wagombea.
Kwa sasa Jaji Njoki Ndung’u mwenye umri wa miaka 60 anasimamia utawala bora na uratibu katika Mahakama ya Juu nchini Kenya .
Mchakato wa upigaji kura
Majaji wa ICC huchaguliwa na mataifa wanachama wakati wa kikao chao cha kila mwaka.
Kuna nchi 125 wanachama.
Kila mwanachama ana haki ya kupiga kura, isipokuwa pale ameamua kutozifuatilia haki hizo.
Uchaguzi ni kwa kura ya siri.
Ili mgombea athibitishwe amechaguliwa anatakiwa kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe waliokuwepo kwenye kikao wakati huo.
Majaji wa ICC huchaguliwa kuhudumu kwa muhula mmoja wa miaka 9, na hawawezi kugombea tena.
















