Polisi nchini Nigeria wameanzisha operesheni ya kuwatafuta wanafunzi kadhaa waliotekwa nyara na wanamgambo wa Boko Haram walipokuwa wakifanya mtihani wa kitaifa (NECO) katika Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa polisi na wakazi waliozungumza na shirika la habari la Anadolu, wanamgambo hao walifika katika Shule ya Sekondari ya Serikali ya Lassa siku ya Jumatatu, iliyopo katika Eneo la Serikali ya Mtaa la Askira/Uba, wakiwa wamevaa sare bandia za jeshi na za walinzi wa misitu ili kujifananisha na maafisa wa usalama.
Washambuliaji hao walifyatua risasi na kumuua mwalimu mmoja huku watu kadhaa wakijeruhiwa, kabla ya kuwateka idadi isiyojulikana ya wanafunzi.
Inadaiwa kuwa magaidi hao waliokuwa na silaha nzito waliivamia shule hiyo asubuhi na kuanza kufyatua risasi ovyo kabla ya kuondoka na wanafunzi kadhaa.
Msemaji wa Polisi wa Jimbo la Borno, Nahum Daso, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema vikosi vya usalama vimetumwa kuokoa waliotekwa na kuwakamata washambuliaji.
"Majira ya saa tatu asubuhi, magaidi walishambulia Shule ya Sekondari ya Lassa. Walifyatua risasi ovyo. Wanafunzi wengi wametekwa nyara," Daso aliiambia Anadolu kwa njia ya simu.
Aliongeza kuwa vikosi vya usalama vilikabiliana na washambuliaji hao na kwamba Kamishna wa Polisi wa jimbo hilo amemwagiza kamanda wa eneo kuratibu operesheni inayoendelea.
"Kwa sasa wanaendelea na msako wa kuwaokoa waliotekwa," alisema Daso, bila kutaja idadi kamili ya wanafunzi waliotekwa.
Tukio hilo la hivi karibuni limetokea wakati eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria likiendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama licha ya miaka ya operesheni za kijeshi dhidi ya Boko Haram na kundi lililojitenga nalo la ISWAP.
Makundi hayo ya kigaidi yamekuwa yakilenga shule mara kwa mara katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria, na kusababisha utekaji mkubwa wa wanafunzi, ukiwemo ule maarufu wa mwaka 2014 ambapo wasichana wa shule ya Chibok walitekwa katika Jimbo la Borno.
Shambulio la Jumatatu limekuja wiki chache baada ya magaidi kuwateka zaidi ya wanafunzi na walimu 40 kutoka shule tatu katika Eneo la Serikali ya Mtaa la Oriire, Jimbo la Oyo, kusini magharibi mwa Nigeria.
Tukio hilo limezua maandamano nchini kote yakiongozwa na vyama vya wafanyakazi, asasi za kiraia na wanafunzi, huku likifufua wasiwasi kuhusu usalama wa shule nchini Nigeria.

















