| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Uganda inasema inahitaji zaidi ya Dola bilioni moja kusambaza umeme nchini kote
Kulingana na Benki ya Dunia kufikia 2023, ni asilimia 51.5 pekee ya watu waliunganishwa na huduma ya umeme nchini Uganda.
Uganda inasema inahitaji zaidi ya Dola bilioni moja kusambaza umeme nchini kote
Wabunge nchini Uganda wanalalamika kuwa wakazi wengi hawana umeme. / Reuters
tokea masaa 3

Uganda inasema ufadhili mkubwa unahitajika ili kufanikisha usambazaji kamili wa umeme nchini humo.

Waziri wa Nchi anayeshughulikia Nishati, Okaasai Opolot, alisema Uganda inahitaji zaidi ya Dola bilioni 1 (takribani shilingi trilioni 4) ili kusambaza umeme kikamilifu nchini, akibainisha kuwa usambazaji mkubwa wa umeme vijijini kwa sasa unasimamiwa na wafadhili.

"Kwa kweli tunategemea wafadhili kuipatia nchi hii umeme, fedha nyingi tunazotumia kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini zinatoka kwa wafadhili na zinakuja na masharti," aliliambia Bunge.

Alikuwa akichangia hoja zilizotolewa na wabunge mbalimbali kuhusu ucheleweshaji wa mpango wa usambazaji umeme vijijini.

Mbunge mmoja, William Chemonges alisema upatikanaji wa umeme ni muhimu kwa maisha ya kila siku kwa jamii nyingi na wananchi katika maeneo yao wanaendelea kuuliza, kwa nini hawana umeme.

Mbunge mwengine Stella Ayang alisema baadhi ya jamii zina nyaya ya umeme lakini zimesalia gizani.

Anyang aliibua wasiwasi juu ya ukosefu wa transfoma katika mkoa wa Karamoja, akisema maeneo mengi yana nyaya za umeme lakini wakazi hawawezi kupata umeme kutokana na kukosa vifaa.

Waziri wa Nchi anayehusika na Nishati alisisitiza kuwa masharti yaliyowekwa na wafadhili yanaelekeza jinsi mpango wa usambazaji umeme unavyotakiwa kutekelezwa hivyo basi kupunguza kasi ya maendeleo.

"Kwa mfano Benki ya Dunia itakuja na mahitaji ya fidia kila tunapopitisha umeme, iwe tunakata mti au hata kuweka miundombinu kwenye ardhi ya mtu. Tusipokubaliana kuondoa mahitaji hayo, chochote tunachofanya kitakuwa kigumu sana kutekeleza," alisema.

Kulingana na Benki ya Dunia kufikia 2023, ni asilimia 51.5 ya watu walikuwa wameunganishwa na huduma ya umeme nchini Uganda.

CHANZO:TRT Swahili