Takriban watu tisa wafariki baada ya kimbunga Gezani kupiga Madagascar
Wakazi wa maeneo hayo ya Toamasina walielezea athari ya kimbunga hicho.
Kimbunga cha Tropiki cha Gezani kiligonga pwani ya mashariki mwa Madagascar, na kuua watu tisa katika jiji hilo la pili kwa ukubwa kwenye kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, huku mvua kali na upepo ukisababisha uharibifu mkubwa, kwa mujibu wa mamlaka ya nchi hiyo.
Ofisi ya usimamizi wa maafa ya Madagascar ilisema watu 19 wamejeruhiwa na takriban wakazi 1,500 walihamishwa katika wilaya ya karibu na mji wa bandari wa Toamasina baada ya kimbunga kupiga eneo hilo.
Wakazi wa maeneo hayo ya Toamasina waliielezea athari ya kimbunga hicho.
"Sijawahi kuhisi upepo mkali kiasi hiki... Milango na madirisha yameharibiwa," alisema Harimanga Ranaivo.
Hiki kilikuwa kimbunga cha pili kugonga Madagascar mwaka huu, siku 10 baada ya kimbunga cha tropiki Fytia kuua watu 14 na kusababisha zaidi ya watu 31,000 kuhama, kwa mujibu wa ofisi ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
Upepo mkali
Gezani pia iliambatana na upepo mkali uliokuwa na kasi ya takriban kilomita 185 kwa saa (115 maili kwa saa), na mawimbi ya upepo yalifikia karibu kilomita 270 kwa saa — huku ukiezua paa na kuangusha miti.
Kabla ya kimbunga kuwasili, serikali ilifunga shule na kuandaa makazi ya dharura.
Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Madagascar awali ilitahadharisha kuongezeka kwa kiwango cha bahari.
Hata hivyo, kufikia Jumatano asubuhi, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Madagascar ilisema kuwa Kimbunga Gezani kilikuwa kimepungua kasi, na kilikuwa kimeelekea magharibi mwa nchi, takriban kilomita 100 kaskazini ya mji mkuu Antananarivo.
"Gezani itavuka milima ya kati kutoka mashariki hadi magharibi leo, kabla ya kusogea baharini katika Mfereji wa Msumbiji jioni hii au usiku wa leo," ilisema Mamlaka hiyo.