Mamia ya raia wa Burundi walifika kwa wingi katika Ubalozi wa Burundi jijini Nairobi, Kenya, Jumatatu, wakitafuta pasipoti na nyaraka za kusafiria, wakati serikali ya Kenya ilipokuwa ikitarajiwa kuanza operesheni dhidi ya wageni wanaoendesha biashara ndogo.
Foleni ndefu zilionekana nje ya Ubalozi wa Burundi na katika vituo vya karibu vya huduma za mtandao, ambapo watu waliokuwa na vitambulisho, pasipoti na vibali walikuwa wakitafuta nyaraka. Baadhi yao walionekana kujiandaa kurejea Burundi.
Ongezeko hilo la watu lilifuatia agizo lililotolewa na Rais William Ruto Septemba 2, likilenga wageni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo. Ruto amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha Wakenya kupata fursa zaidi za kiuchumi.
“Kuanzia wiki ijayo, wafanyabiashara wote wanaofanya biashara hizo ndogo wanapaswa kuzifunga,” Ruto alisema wakati huo, huku akiweka Septemba 7 kuwa tarehe ya kuanza kwa utekelezaji wa hatua hiyo.
Hata hivyo, serikali ya Kenya baadaye ilifafanua kuwa agizo hilo halimaanishi kupigwa marufuku kwa jumla kwa wafanyabiashara wa kigeni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Korir Sing’Oei, alisema Jumapili kwamba wageni wenye vibali halali vya kufanya kazi na leseni za biashara wanaendelea kulindwa kisheria.
Marufuku si kwa wageni wote
“Tunahakikisha kwamba wafanyabiashara wadogo au wakubwa pamoja na wafanyakazi wa mataifa yote, wenye nyaraka zinazohitajika — vibali vya kazi na leseni — wanalindwa kisheria kuendesha shughuli zao nchini Kenya,” Sing’Oei alisema.
Aliongeza kuwa raia wa Burundi, pamoja na raia wengine wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, wako huru kuishi na kufanya kazi nchini Kenya mradi wanazingatia sheria za nchi hiyo.
Afisa mmoja wa Ubalozi wa Burundi alisema utoaji wa nyaraka za kusafiria ni huduma ya kawaida ya kibalozi na haujaanzishwa mahsusi kutokana na hali ya sasa.
Wizara ya Biashara ya Kenya ilisema wageni wanaoingia nchini kwa utaratibu wa kutohitaji viza au kwa ziara za kitalii hawapati moja kwa moja haki ya kufanya kazi au kuendesha biashara. Ilisema wanapaswa kupata vibali vinavyohitajika, huku ikiongeza kuwa utekelezaji wa sheria utafanywa kwa kuzingatia sheria za Kenya pamoja na nafasi ya nchi hiyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wakati huo huo, polisi waliwaonya Wakenya dhidi ya kuwanyanyasa raia wa kigeni.
Mamlaka zilisema hazijapokea taarifa rasmi kuhusu wimbi la watu kuondoka nchini au mashambulizi yaliyolenga raia wa Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) au Rwanda.
Hata hivyo, matukio hayo yameongeza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa hisia za chuki dhidi ya wageni nchini Kenya kufuatia agizo la Rais Ruto. Agizo hilo lilitolewa wakati kukiwa na mjadala mpana kuhusu raia wa kigeni kushindana na wazawa katika kupata ajira na fursa za biashara ndogo.
Hatua ya Kenya pia imefananishwa na hali hio hio katika nchi jirani ya Tanzania, ambayo mwaka 2025 iliweka vikwazo kwa wasio wazawa kujihusisha na baadhi ya biashara ndogo, pamoja na Afrika Kusini, ambako kampeni dhidi ya wahamiaji na mashambulizi dhidi ya biashara zinazomilikiwa na wageni yamekuwa yakizua wasiwasi mara kwa mara kuhusu chuki dhidi ya wageni.




















