Zaidi ya watu 53 wameuawa na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa kufuatia shambulio la wapiganaji wa kundi la Houthi dhidi ya kituo cha mafunzo ya kijeshi katika mkoa wa Shabwa, kusini mwa Yemen.
Katika taarifa iliyowekwa Jumatatu katika mtandao wa kijamii wa Facebook na Mamlaka za Mkoa wa Shabwa, shambulio hilo lililenga kituo hicho wakati vikosi vipya vya kijeshi wa ndani walipokuwa wakipatiwa mafunzo.
“Ukubwa wa janga hili hauwezi kushughulikiwa kwa kulaani tukio hilo pekee, bali unahitaji hatua za haraka za kijeshi na kiusalama ili kuzuia mashambulio kama haya yasijirudie,” mamlaka za eneo hilo zilisisitiza.
Aidha, mamlaka hizo zimetoa wito kwa serikali ya Yemen pamoja na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuimarisha uwezo wa ulinzi wa mkoa huo ili kukabiliana na mashambulio ya aina hiyo.
Hata hivyo, hadi sasa wapiganaji wa Houthi hawakutoa ufafanuzi kuhusu taarifa hiyo.
Shambulio hilo limetokea wakati ambapo mapigano kati ya wapiganaji wa Houthi na vikosi vinavyounga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa yakiendelea kuongezeka.
Serikali hiyo inaungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Yemen imekuwa katika hali ya mzozo tangu mwaka 2014, wakati wapiganaji wa Houthi walipoiteka mji mkuu, Sanaa, pamoja na maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi hiyo.




















