Tanzania imeporomoka hadi nafasi ya 113 duniani toka ile ya 111, kwa ubora soka, kulingana na orodha mpya iliyotolewa na FIFA, Aprili 1, 2026.
Tanzania ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Liechtenstein kwenye michuano ya FIFA Series iliyofanyika hivi karibuni nchini Rwanda, licha ya baadaye kuja kuifunga Macau, bao 6-0.
Kwa upande wao, Kenya wamepanda kwa nafasi mbili kwenye orodha ya FIFA, kutoka ya 113 hadi 111 duniani, baada ya kushinda mchezo wake dhidi ya Grenada kwenye michuano hiyo hiyo.
DRC, ambayo imetoka kufuzu michuano ya Kombe la Dunia kwa mwaka 2026, imeendeleza ubabe wake wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikishika nafasi ya 46 duniani.
Uganda ipo katika nafasi ya 80, ikifuatiwa na Rwanda ambayo inashika nafasi ya 128, wakati Burundi ikiwa ni ya 142 duniani.
Kulingana na orodha hiyo ya FIFA,Sudan Kusini inashika nafasi ya 170 huku Somalia ikishika mkia katika nafasi ya 198.











