Tanzania: Rais Samia atoa Milioni 100 kwa ujenzi wa makumbusho ya Magufuli
Magufuli, au JPM kama alivyoitwa na wengi, alifariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, kwa maradhi ya moyo.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, ametoa shilingi za Kitanzania milioni 100, ili zikamilishe ujenzi wa makumbusho wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, John Pombe Magufuli yaliyopo Chato Mkoani Geita.
Akizungumza kwenye Ibada ya kumbukizi ya miaka 5 ya kifo cha kiongozi huyo, iliyofanyika Machi 17, 2026, Makamu wa rais wa nchi hiyo, Emmanuel Nchimbi amesema kuwa, kwa kutambua mchango wa Hayati Magufuli kwenye uongozi wa taifa hilo, Rais Samia ameweka jicho lake karibu na maendeleo ya ujenzi wa makumbusho hiyo iliyopo Chato, mkoani Geita.
“Kwa kutambua na kuenzi mchango wa Hayati John Pombe Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa makumbusho yake hapa Chato, na ametaarifiwa kwamba, ili ujenzi huo ukamilike, zimepungua Shilingi Milioni 100 za Kitanzania…nafurahi kuwajulisha kuwa mheshimiwa rais ameamua kutoa fedha hizo zote ili kukamilisha kazi hiyo,” alisema Nchimbi.
Makumbusho hayo yanakusudiwa kuwa sehemu muhimu ya kuhifadhi historia ya maisha, uongozi na mafanikio ya Hayati Magufuli, ambapo vizazi vya sasa na vijavyo vitapata fursa ya kujifunza na kuelewa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania.
Magufuli, au JPM kama alivyoitwa na wengi, alifariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, kwa maradhi ya moyo.