Watanzania wanakumbuka miaka 5 toka walipompoteza John Pombe Magufuli, aliyekuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Magufuli, au JPM kama alivyoitwa na wengi, alifariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, kwa maradhi ya moyo.
Tanzania na dunia nzima itamkumbuka Magufuli kwa kuweka msisitizo kwenye nidhamu ya kazi, miradi mikubwa ya maendeleo, na kupambana na ufisadi.
Chini ya utawala wake, Magufuli alianzisha Mahakama Maalum ya Kushughulikia Rushwa na Ufisadi, hatua iliyolenga kupunguza rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, pamoja na kuimarisha uwajibikaji.
Akiongozwa na kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’, rais Magufuli alipania kuongeza kasi ya kusikiliza kesi kubwa za ufujaji wa mali za umma na rushwa.
Sifa za kiongozi huyo zilivuka mipaka ya nchi yake, hasa kutokana na msimamo wake wa kupinga uonevu na kuwatetea wananchi wanyonge.
Atakumbukwa pia, kwa kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa umma walioonekana kuwaonea wananchi au kwenda kinyume na maadili, ikiwa ni pamoja na kuingilia kati kero za wafanyabiashara.
Yote tisa, kumi ni miradi ya maendeleo aliyoiasisi chini ya utawala wake, ambayo bado inaendelea kuifanya Tanzania izidi kung’ara kikanda na hata kimataifa.
Moja ya miradi hiyo, ni pamoja na Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Kisasa ya SGR, ambao ulikuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mingine.
Wakati wa utawala wake, Magufuli alifanikiwa kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), mpango ambao ulihusisha ununuzi wa ndege mpya kadhaa kama vile Boeing 787-8 Dreamliner, Airbus na Bombardier Q400, ili kuimarisha sekta ya anga na utalii.
Magufuli atakumbukwa kwa ujenzi wa madaraja ya kisasa jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari.
Moja ya madaraja hayo ni pamoja na la ‘Ubungo Interchange’, Daraja la Tanzanite na lile la Kigongo- Busisi, maarufu kama daraja la JPM.
Hata hivyo, wako baadhi ya watu waliopinga baadhi ya sera zake, ikiwemo kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na kuminya uhuru vyombo vya habari.

















