Upinzani Tanzania wasema mamia wameuawa, UN yataka uchunguzi ufanyike

Waziri wa Mambo ya Nje Mahmoud Thabit Kombo, amekanusha madai ya upinzani ya kwamba mamia wameuawa.

Waandamanaji nchini Tanzania wamejitokeza kupinga shughuli za uchaguzi. / / Reuters

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kimesema siku ya Ijumaa kwamba mamia ya watu wameuawa katika maandamano ya kupinga shughuli za uchaguzi zilizofanyika wiki hii, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, akitoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu madai ya serikali kutumia nguvu za kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Aidha, Shirika la Umoja wa Mataifa limesema taarifa za kuaminika zinaonyesha kwamba takriban watu 10 wameuawa katika maandamano yaliyotokea katika miji mitatu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa taasisi ya kimataifa kutoa idadi ya makadirio ya vifo tangu uchaguzi uanze.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mahmoud Thabit Kombo alipohojiwa na shirika la habari la Reuters, amesema idadi ya vifo iliyotolewa na upinzani si ya kweli, akisisitiza ya kwamba serikali bado haiwezi kuthibitisha idadi ya watu waliouawa. Waziri huyo pia alikanusha madai kwamba maafisa wa usalama wametumia nguvu kupita kiasi.

SOURCE: Reuters