Serikali ya Tanzania yasema hali ya kawaida itarejea hivi karibuni
Kwa mara ya kwanza serikali ya Tanzania imezungumzia kuhusu machafuko yanayoendelea kwa njia ya ujumbe kutoka wizara ya mambo ya nje kwa wanadiplomasia wa nchi za nje kupitia televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.
Serikali ya Tanzania yasema hali ya kawaida itarejea hivi karibuni
Maandamano yalizuka 29 Oktoba 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu / Reuters
tokea masaa 11

Serikali ya Tanzania siku ya Ijumaa ilipuuzilia mbali maandamano ambayo yametikisa miji kadhaa tangu uchaguzi mkuu mapema wiki hii kama "matukio ya hapa na pale" na kusema kuwa inajitahidi kurejesha hali ya kawaida haraka.

Maandamano yalizuka 29 Oktoba 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Wengi wakiwa na hasira kuhusiana na kutengwa kwa wapinzani wawili wakuu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kinyang'anyiro hicho na kile ambacho wakosoaji wa serikali wanasema ni ukandamizaji.

Polisi wametangaza amri ya kutotoka nje usiku kucha katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam siku mbili zilizopita baada ya ofisi za serikali na majengo mengine kuchomwa moto, na huduma za mtandao kuzimwa tangu Jumatano.

Hakujawa na idadi rasmi waliouawa kwenye maandamano hayo au taarifa za majeruhi zilizothibitishwa, lakini chanzo cha kidiplomasia kilisema kulikuwa na ripoti za kuaminika za vifo kadhaa.

Kwa mara ya kwanza serikali ya Tanzania imezungumzia kuhusu machafuko yanayoendelea kwa njia ya ujumbe kutoka wizara ya mambo ya nje kwa wanadiplomasia wa nchi za nje kupitia televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.

Wizara iliwafahamisha kuwa, "kutokana na matukio ya hapa na pale ya uvunjaji wa sheria na usalama, serikali imeimarisha ulinzi na kuchukua hatua kadhaa za tahadhari", ilisema. "...hatua za usalama zilizopo ni za muda lakini ni muhimu na hali ya kawaida itarejea hivi karibuni."

Wanajeshi na polisi walishika doria barabarani na kuweka vizuizi siku ya Ijumaa.

Serikali iliwataka wafanyakazi wa umma kufanyia kazi kutoka nyumbani na kuwataka wengine ambao hawana sababu ya dharura pia kufanya kazi nyumbani.

Machafuko hayo yanaleta changamoto kwa Rais Samia, ambaye alijizolea sifa baada ya kuingia madarakani mwaka 2021 kwa kupunguza kile kinachoonekana kuwa ukandamizaji wakati wa uongozi wa mtangulizi wake John Pombe Magufuli lakini hivi karibuni ameshutumiwa kwa kuwabana wakosoaji pamoja na kamata kamata na kutekwa nyara kwa wapinzani.

Rais Samia amekanusha madai ya ukiukwaji wa haki.

Alisema mwaka jana aliagiza uchunguzi ufanyike kuhusu taarifa za utekaji nyara, lakini hakuna matokeo rasmi yaliyotolewa.

Tume ya uchaguzi ilianza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi siku ya Alhamisi, ambayo yalionyesha Rais Samia akiongoza kwa kura nyingi katika maeneo kadhaa.

Hussein Mwinyi, rais wa Zanzibar, ambaye naye ni wa Chama tawala Cha Mapinduzi (CCM), alichaguliwa tena kwa zaidi ya asilimia 74 ya kura, Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilitangaza.

Akizungumza kwenye kituo cha habari cha serikali siku ya Alhamisi, Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda alisema majeshi na vyombo vingine vya usalama "yamedhibiti hali hiyo".

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kilitoa wito wa maandamano wakati wa uchaguzi huo.

Chama hicho kilienguliwa mwezi Aprili baada ya kukataa kusaini kanuni za maadili na kiongozi wake Tundu Lissu kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Tume ya uchaguzi pia ilimuengua mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, na kumuacha Samia akabiliane na wagombea wa vyama vidogo vidogo.

Katika taarifa siku ya Alhamisi, wajumbe wa Bunge la Ulaya waliutaja uchaguzi huo kuwa "usiyo huru", wakisema "ulijitokeza katika mazingira ya ukandamizaji, vitisho na hofu".

CHANZO:TRT Afrika and agencies