Machafuko Tanzania yaathiri biashara Rwanda

Maandamano katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yameathiri baadhi ya huduma, ikiwemo usafiri wa malori yanayopeleka bidhaa nje ya nchini na bidhaa kutoka nje kukwama.

Waandamanaji jijini Dar es Salaam. / Reuters

Vurugu zinazoendelea nchini Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu wa 29 Oktoba 2025, zinatatiza usafirishaji wa bidhaa zinazopelekwa Rwanda, huku madereva wa malori wakieleza kuhusu kupotea kwa mawasiliano, uhaba wa mafuta na kukawia sana katika barabara kuu.

Nchi hiyo ya Tanzania ambayo ni jirani ya Rwanda imekumbwa na vurugu tangu 29 Oktoba 2025, siku ya Uchaguzi Mkuu, huku baadhi ya wananchi wakiingia mitaani kupinga matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais ambayo yalimrejesha madarakani Samia Suluhu.

Maandamano hayo yameathiri baadhi ya huduma, ikiwemo malori yanayosafirisha bidhaa kupitia mpakani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva wa Malori wa Rwanda, Noel Nkurikiye, aliambia New Times Rwanda, chombo vya habari nchini humo, kuwa hali inazidi kuwa mbaya kutokana na vurugu kuenea katika mikoa mikubwa ya Tanzania.

"Hakuna mawasiliano," alisema.

"Madereva kwa kawaida huwasiliana na waajiri wao kwa ajili ya uratibu, hasa wanapohitaji kujaza mafuta, lakini hilo haliwezekani tena. Wengi wao waliishiwa na mafuta na kulazimika kusimama pale walipokuwa."

Alisema vurugu hizo zilizoanzia miji ya Dar es Salaam na Dodoma, sasa zimefika eneo la Kahama karibu na Rwanda, na kuwalazimisha madereva wa mizigo kutoka Rwanda kusimamisha au kubadilisha njia.

"Katika siku za mwanzo za maandamano, malori yangeweza kusafiri hadi kufika maeneo ambayo hayakuwa salama tena. Sasa yamekwama katika maeneo ambayo sio mbali sana na mpaka."

Nkurikiye alisema kushindwa kuwasiliana na madereva bado ni tatizo kubwa. "Hatupata njia ya kuwasiliana nao," alisema.

Alisisitiza kuwa usumbufu huo unaleta changamoto kubwa kwa biashara ya Rwanda, ikizingatiwa kwamba bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje zinategemea Bandari ya Dar es Salaam ya Tanzania, ambayo iko takriban kilomita 1,500, kuliko Bandari ya Mombasa, iliyo umbali wa takriban kilomita 1,800 kupitia Uganda.

"Dar es Salaam ndiyo bandari tunayotumia zaidi, kwa sababu ni karibu na yenye ufanisi zaidi," alisema.

"Hata bidhaa zinapokuja Mombasa, mara nyingi tunapendelea kupitia Tanzania badala ya Uganda ili kuepuka vituo vingi vya mizani na kupunguza muda wa kusafiri."

Alieleza kuwa malori yanayopitia Tanzania kutoka Mombasa yanapitia vituo sita vya mizani (viwili nchini Kenya na vinne Tanzania), huku yale yanayotumia njia ya Uganda yakipitia vituo kumi na mbili kwa jumla.

"Baadhi ya malori ambayo tayari yalikuwa yameondoka Mombasa kuelekea Rwanda kupitia Tanzania yalilazimika kurejea na kupitia Uganda," Nkurikiye alisema.

"Mizigo ambayo bado iko njiani na inayotarajiwa kwenda Dar es Salaam inatakiwa kuelekezwa Mombasa haraka iwezekanavyo ili kuepuka Rwanda kukumbwa na uhaba wa bidhaa muhimu. Wasafirishaji pia wanatakiwa kutumia bandari hiyo ya Mombasa."