Vurugu za baada ya uchaguzi zashuhudiwa Tanzania
Baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yameshuhudia vurugu baada ya uchaguzi, huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (INEC) ikiendelea kutangaza matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Vurugu za baada ya uchaguzi zashuhudiwa Tanzania
Waandamanaji jijini Dar es Salaam. / Reuters

Uwepo wa magari ya vikosi vya ulinzi na usalama umegeuka kuwa jambo la kawaida katika miji mbalimbali nchini Tanzania, kufuatia vurugu zilizoibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 2025.

Jijini Dar es Salaam, maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameendelea kuzunguka mitaa mbalimbali ya jiji hilo kubwa kibiashara nchini humo, huku polisi, hususani wale kutoka kikosi cha kutuliza ghasia, maarufu kama ‘FFU’, wakifanya doria za hapa na pale.

Hata hivyo, yapo baadhi ya maeneo ya jiji hilo ambayo yameendelea kushuhudia milio ya risasi na moshi kutoka mabomu ya kutoa machozi.

Wakati hayo yote yakiendelea, bado biashara zimeendelea kufungwa, huku watumishi wa umma na wanafunzi wakilazimika kubaki majumbani kutokana na hali ya usalama kutotengemaa.

“Hali bado si shwari, kuna nyakati tunasikia milio ya risasi na mabomu ya machozi, uwepo wa vikosi vya kulinda usalama bado vinaendelea kufanya doria zao,” anasema Emmanuel Kimolo, mwendesha Bajaji wa jijini Dar es Salaam, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Kimolo, ambaye amelazimika kuhamia Sinza kwa muda kutoka makazi yake rasmi ya Kibamba, anasema kwamba ameshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto na baadhi ya waandamanaji, hali inayoashiria kuwa usalama bado haujatengemaa.

“Hali bado ni tete, kwa mfano hakuna mabasi barabarani, kuna waliopo mikoani wameshindwa kurudi jijini Dar es Salaam,” anaeleza.

Kwa upande mwingine, hali kama hiyo imeshuhudiwa kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha na Dodoma.

Kwa mfano, jiji la Arusha ambalo ni kitovu cha biashara kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, jumla ya vituo vya polisi vitatu, viliripotiwa kuchomwa moto na waandamanaji, huku hoteli maarufu ya SnowCrest ikiharibiwa vibaya.

Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi zozote za vifo au majeruhi zilizoripotiwa huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (INEC) ikiendelea kutangaza matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Jijini Dodoma, hali ya usalama imezidi kuimarishwa baada ya baadhi ya waandamanaji kujaribu kuvamia makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), saa chache baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.

Bado haijafahamika sababu za watu hao kujaribu kuvamia makao makuu ya chama hicho tawala nchini Tanzania.