Leah ameanza na panya 10 lakini sasa hivi ana panya zaidi ya 200. Picha/TRT Afrika.

Na Mwandishi wetu

TRT Afrika, Morogoro, Tanzania

Ufugaji wa panya weupe wanaojulikana kitaalamu kama “White albino rat” kutokana na muonekano wao, umeanza kushamiri mkoani Morogoro nchini Tanzania.

Leah Pangapanga mkazi wa Morogoro amekuwa akifuga panya kibiashara kwa zaidi ya mika mitano sasa.

Anasema alianza na panya kumi tu ambao aliwapata kwa rafiki yake, lakini ndani ya muda mfupi walizaliana na kufika zaidi ya 200. “Hawa panya wanazaliana sana. Akibeba mimba baada ya siku 28 anazaa watoto mpaka 12 na ndani ya muda mfupi anaweza kubeba mimba nyengine,” anasema.

Nchini Tanzania, ingawa kuna baadhi ya makabila ambayo yanakula panya, lakini panya sio wa kula, bali hutumika zaidi kwenye tafiti za kisayansi kwenye vyuo na shule za sekondari hasa kwenye majaribio ya kibiolojia. Hii ni kwa sababu, wataalamu wanasema, mfumo wa panya unafanana kwa kiasi kikubwa na ule wa binadamu.

Leah, anasema panya anaowafuga ni tofauti na wale weuse wanaopatikana majumbani au vichakani. Picha/TRT Afrika. 

Kama ilivyo kwa ufugaji wa kuku ambao chakula chao kikubwa ni pumba, panya nao wanakula pumba ambazo zinakuwa na mchanganyiko maalumu wenye virutubisho vya kutosha vinavyowasaidia kukuwa kwa kasi inayotakiwa. Mchanganyiko huo mara nyingi unahusisha pumba, dagaa, uduvi, na hata viambata vya vitamini na maziwa ya unga ili kuchochea uzalishaji.

Jamii imekuwa na mtizamo hasi kuhusu panya. Wamekuwa wakinasibishwa na usambazaji wa maradhi hasa vimelea vya tauni na kusababisha uharibifu maeneo mbalimbali. Hata hivyo, Leah, anasema panya anaowafuga yeye ni tofauti na wale weuse wanaopatikana majumbani au vichakani.

"Nilipoanza kuwafuga jamii iliniona kama mtu aliyechanganyikiwa, kwa sababu tayari nilikuwa mfugaji mkubwa wa kuku ambao baadae niliuacha kutokana na magonjwa na gharama za uendeshaji tofauti na ilivyo kwa panya ambao nawalisha mara moja tu kwa siku na hawahitaji uangalizi mkubwa kama kuku, na bado faida haipishani na ile niliyokuwa napata wakati wa kufuga kuku," anasema Leah.

Kwa mujibu wa Leah, soko la panya huwa ni la msimu hasa nyakati ambazo kuna mitihani ya majaribio ya sayansi ambapo panya mmoja huuzwa kwa wastani wa dola mbili za kimarekani ambazo ni sawa shilingi 4 mpaka elfu 5 za Kitanzania.

"Manunuzi hufanyika kwa mkupuo. Mteja mmoja anaweza kununua panya 200 mpaka 300 kwa wakati mmoja," anasema.

Panya weupe wanaojulikana kitaalamu kama “White albino rat” kutokana na muonekano wao. Picha/TRT Africa.

Soko Jipya

Siku za hivi karibuni kumeibuka soko jipya ambalo linaleta matumaini zaidi katika biashara hii ya ufugaji panya.

"Maeno tengefu ya kuhifadhi wanyama pori “ZOO” ambao mara kadhaa hutumia panya kama chakula cha nyoka ambao wana wafuga," amesema Leah.

Mara kadhaa Leah amekua akishindwa kuwahudumia ipasavyo wateja wake wote kutokana na kuwa na idadi ndogo ya panya. Hii ina maana kwamba, mahitaji ya soko ni makubwa kuliko uwezo wake wa kuhudumia.

Ni kutokana na changamoto hiyo, hivi sasa ameanza kuwashawishi na kuwashirkisha wanawake wengine ili nao waanze kufuga panya kutokana na ufugaji wake kuwa wepesi.

"Mimi nawapenda sana wanawake wenzangu, hivyo nikiona fursa nawashirikisha ili tufanikiwe pamoja,” anasema.

Hata hivyo, Leah anakiri kwamba, licha ya kuwepo kwa jitihada hizo, lakini bado hawajaweza kukidhi mahitaji ya soko yanayoendelea kuongezeka siku hadi siku kutokana na kufunguliwa kwa shule mpya na hata kuongezeka kwa majaribio ya kisayansi.

"Nilipoanza kuwafuga jamii iliniona kama mtu aliyechanganyikiwa, kwa sababu tayari nilikuwa mfugaji mkubwa wa kuku ambao baadae niliuacha kutokana na magonjwa na gharama za uendeshaji tofauti na ilivyo kwa panya ambao nawalisha mara moja tu kwa siku na hawahitaji uangalizi mkubwa kama kuku, na bado faida haipishani na ile niliyokuwa napata wakati wa kufuga kuku."

Leah Pangapanga, mkazi wa Morogoro, Tanzania

Kwa mujibu wa taasisi ya SUGECO ambayo inaundwa na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, ufugaji wa panya weupe ni rafiki na si hatarishi kwa afya za wafugaji wala mazingira kutokana na kufungwa kwenye mabanda. Wataalamu hao, wanasema, muhimu ni kuzingatia usafi wakati wote lakini pia kuwapa dawa muhimu kama vile za minyoo na za kuua viroboto mara kwa mara.

Wakati Leah na wenzake wakiendelea kuvuna matunda ya ufugaji panya, kibarua kinachowakabili ni jinsi ya kuishawishi jamii kuamini kwamba, ufugaji wa panya ni salama na una tija ya kiuchumi.

TRT Afrika