Wabunge wa Uganda wakiwa katika Bunge la nchi hiyo. 

Bunge la Uganda limejadili kuajiriwa kwa watu wasio raia kuwa viongozi wa benki nchini humo.

Wabunge wamedai kuwa, haifai kwa wageni kupewa kazi hizo iwapo kuna wananchi wa Uganda wenye ujuzi wa kufanya kazi hizo.

“Nataka kuunga mkono Benki Kuu kwa kumkataa mtu ambaye si raia wa Uganda ambaye aliteuliwa kwa sababu Benki inapofanya vizuri sasa wanataka kuirudisha wenyewe," Thomas Tayebwa, naibu Spika wa Bunge la Uganda amesema.

Mjadala huu umetokea huku Benki Kuu ya Uganda, ikikataa kuidhinishwa kwa raia wa kigeni ambae ameajiriwa kuwa Afisi Mkuu Mtendaji wa Benki ya Stanbic Uganda.

Stanbic ni benki ya kimataifa yenye asili yake Afrika Kusini. Tawi lake la Uganda, lilikuwa likiongozwa na raia wa Uganda, Patrick Mweheire lakini sasa nafasi hiyo iko wazi.

"Kwa kawaida, raia wa kigen huajiriwa iwapo tu hakuna raia katika nchi mwenye kukidhi vigezo. Standard Bank Group na Benki ya Stanbic zinaweza kuwa hazijatafuta Waganda wenye uwezo wa kuendesha benki hiyo, lakini ninaamini wapo," Paul Omara, mbunge wa kaunti ya Otuke aliambia Bunge.

Wabunge wamesema ni wakati muafaka wa Uganda kujiunga na mataifa kama Kenya na Afrika Kusini kuzuia nafasi hizo zenye faida kwa raia wao wenyewe, ili kuwalinda wafanyakazi wa Uganda.

"Sasa suala la kumleta mtu asiye raia wa Uganda kwenye benki ambayo tulikabidhi mali zetu kubwa na pesa zetu nyingi, utajiuliza kwanini? Rais wa uganda wangekuwa wanafanya vibaya, ingekuwa ni changamoto," Naibu Spika wa Bunge ameongezea.

"Hakuna mgeni anayeweza kwenda Kenya na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki. Afrika Kusini ambako Stanbic inatoka, hakuna mgeni ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki yoyote, kwa nini Uganda?” Tayebwa aliuliza.

Benki ya Stanbic Uganda haijatoa taarifa yoyote kufuatia majadiliano ya Jumanne ya Bunge.

TRT Afrika