Uganda imeanza kampeni ya chanjo dhidi ya homa ya manjano, yaani yellow fever.
Wizara ya Afya ya Uganda imezindua zoezi hilo ambalo litaendeshwa katika wilaya 53 nchini kote hadi Aprili 8.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, hii ni awamu ya pili ya kampeni ya taifa ya kutokomeza homa ya manjano.
Kampeni hiyo inalenga maeneo ndani ya ukanda, unaozunguka bara la Afrika, na Uganda ni kati ya nchi 29 zilizo katika hatari kubwa ya homa ya manjano.
Kampeni hii inalenga angalau raia milioni 14.5 kati ya umri ya mwaka mmoja na miaka 60.
Homa ya manjano ni ugonjwa wa virusi unaoenezwa kwa kuumwa na mbu walioambukizwa ambao hupatikana zaidi katika sehemu za Amerika Kusini na Afrika.
"Ni maambukizi ya virusi na inaua, kwa hivyo ukipata chanjo na kwa bahati mbaya upate homa ya manjano siku za usoni mwili wako utakuwa na kinga," amesema Dkt, Diana Atwine , Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Uganda.
Wasipopewa watu, virusi vya homa ya manjano vinaweza kuharibu ini na viungo vingine vya ndani na kuwa hatari.
Wanawake wote wajawazito wameshauriwa kusubiri hadi baada ya kujifungua ili kupata Chanjo ya Homa ya Manjano.
"Pia Wizara imeshauri watu kuchukua hatua za kiusalama kama vile kutumia chandarua kila usiku, kusafisha vichaka vilivyo karibu ya nyumba na kutumia dawa za mbu," Wizara ya Afya imesema.
"Uganda ipo katika eneo tunaloliitwa ukanda wa homa ya manjano na kwa vile tuna mbu basi chanjo katika maeneo haya ndiyo njia muafaka ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huu. Chanjo moja tu inakupa kinga ya maisha," Dkt. Daniel Kyabanze, Mkurugenzi katika Wizara ya Afya ya Uganda ameelezea.
Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kuwa kuna maambukizi 200,000 vya homa ya manjano ulimwenguni kila mwaka, na kusababisha vifo 30,000.