Kundi hili la wasanii linasema linanuia kutumia densi kusambaza ujumbe wa amani  Picha: Inuka   

Na Kudra Maliro

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekumbwa na mapigano makali ya kivita kwa miaka mingi, na athari kubwa za kisaikolojia kwa idadi ya watu haswa wanawake na watoto.

Kasereka Kasolene, kijana mcheza dansi, amekuja na suluhu ya kipekee. Anatumia ustadi wake wa kucheza ili kuwapa watu faraja wakati wa vita. Mcheza densi huyo mwenye umri wa miaka 23 alianza kuiga magwiji wa Marekani kama vile Michael Jackson na Chris Brown, alipokuwa na umri wa miaka 8.

"Nilianza taaluma yangu katika densi ya kisasa mnamo 2016. Nilichaguliwa kusomea densi ya kitamaduni na ya kisasa ya Kiafrika katika Ecole Sables nchini Senegal kwa miaka mitatu," aliiambia TRT Africa.

Kasolene na kundi lake wanajaribu kuwasilisha ujumbe wa amani kupitia densi katika mji wa Goma mashariki mwa nchi. Wanatoa maonyesho katika maeneo ya umma kama vile sokoni na barabarani ili kuburudisha na kuhamasisha watu walioathiriwa na vurugu katika eneo ambalo milio ya bunduki na silaha nyingine ni mara kwa mara.

Uelewa wa kihisia

Kikundi cha densi cha Inuka huwaleta pamoja vijana kadhaa wanaotumia sanaa hiyo kama njia ya matibabu.

Wanadensi hao wamepata umaarufu mjini Goma na miji ya karibu. Picha: Inuka 

"Tunapocheza na watoto ambao wamepatwa na kiwewe, wanasahau, kwa sababu densi inawasaidia kushinda maumivu ya kimhemko na kuwafanya wafikirie kitu kingine isipokuwa ukatili wa vita waliopitia, haswa wale wa Kivu Kaskazini," anasema Abdoul Tambwe, mcheza densi wa kundi la Inuka.

"Kutokana na vipindi vya dansi vya kikundi cha Inuka, watoto hujitambua vyema na kuelewa vyema hisia zao. Kupitia densi, wanaweza kuelezea hisia zao kimwili na kimawazo kupitia njia za kuburudisha. Miondoko ya densi pia huwaruhusu kufanyia mwili mazoezi na kuchangamsha damu ," anasema.

"Vipindi vyetu vya ngoma ni tiba kwa watoto. Inawasaidia kukuza kujiamini na kujistahi, kwa sababu wao ndio viongozi wa baadaye wa Kongo,” anasema Bw. Tambwe.

“Kama msanii jukumu langu ni kutoa matumaini na kuongeza uelewa kwa watu wetu ili tuepuke migogoro baina ya jamii ambayo imegharimu maisha ya watu wengi,” anaongeza.

Ngoma bila mipaka

Jeshi la Kongo na washirika wake wamekuwa wakiendesha operesheni mashariki mwa DR Congo kwa miezi kadhaa katika jaribio la kuwatimua waasi wa M23 kutoka eneo hilo. Maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia hizo wanaishi katika kambi karibu na mji wa Goma.

Sanaa inaaminiwa kuwa muhimu sana katika kuimarisha afya ya akili . Picha: Inuka 

Kwa Kasolene, sanaa haina mipaka. Anahakikisha kuwa hana tatizo na mataifa mengine licha ya mzozo uliopo kati yao na DRC.

Kwa sasa Kasolene anashiriki katika Tamasha la Ngoma linaloendelea mjini Goma na wacheza densi kadhaa kutoka Rwanda, Burundi na nchi nyingine zinazopakana na DRC. Tamasha hili la densi linalenga kukuza utangamano kwa amani na majirani kw alengo la kupunguza mivutano.

DRC ina idadi kubwa ya vijana huku asilimia 60 wakiwa chini ya miaka 20. Picha: Inuka 

"Tulitaka kuuonyesha ulimwengu kuwa DRC na Rwanda ni nchi mbili zenye undugu na urafiki," anasema Bw. Batumike, mwandaaji wa Tamasha la Dansi huko Goma.

Anaeleza kuwa wacheza densi wa Rwanda na Congo walikusanyika kwa zaidi ya wiki moja mjini Goma, wakifanya mazoezi pamoja na kushiriki jukwaa.

Kasolene na kikundi chake wanapanga kutembelea kambi za watu waliohamishwa karibu na Goma ili kufundisha ngoma na kuwasaidia watu waliohamishwa kutoka makwao kuondokana na kiwewe kinachohusiana na migogoro.

Wasanii hao pia wanafanya uhamasishaji na kutoa wito wa maji safi katika utendaji wao. Picha: Inuka

"Lengo ni kuzuia watoto wanaoishi katika kambi hizi kuishia mitaani. Wakiweza kucheza vizuri, wataweza kujitunza", anaeleza.

"Tunajaribu kuonesha taswira chanya ya DRC kupitia dansi na tunatumai kuwa katika miezi michache, hatutazungumza juu ya Congo Mashariki kama eneo la migogoro bali talanta ambayo ukanda huu hutoa. Sisi ni wasanii na tunawa elimisha watu wengi,” anamalizia Bw. Kasolene.

TRT Afrika