Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi / Photo: AA

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Felix Antoine Tshisekedi Tchilombo ni rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Anatetea nafasi yake ya urais kwa muhula wa pili katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 20 Disemba mwa huu. Hii ni baada ya kuhudumu miaka mitano ya mwanzo ya kuongoza taifa hilo kubwa lakini lenye migogoro ya kivita hasa eneo lake la mashariki.

Felix Tchisekedi, Mtoto wa Baba

Huwezi kumzungumzia Felix Tchisekedi bila kumtaja baba yake Étienne, aliyekuwa mwanasiasa mkongwe nchini humo.

Felix Tchisekedi alizaliwa tarehe13 Juni 1963 mjini Kinshasa akiwa mtoto wa 3 kwenye familia ya watoto watano.

Felix Tshisekedi alihudumu katika kivuli cha baba yake hadi kurithi chama cha 'Union pour la Démocratie et le Progrès Social' UDPS baada ya baba yake kufariki dunia mwaka 2017.

Baadae Felix Tchisekedi alijijengea umaarufu wa kisiasa hadi kuwa mtetezi wa chama hicho katika uchaguzi wa urais wenye utata wa mwaka wa 2018.

Felix Tshisekedi rais wa DRC.

Mapema ''Fatshi Béton '' jina lake la utani, alionekana kuwa karibu na mtangulizi wake Joseph Kabila na kuunda muungano kabla ya viongozi hao kuhitilafiana hadi kutengana kabisa kisiasa.

Mwaka wa 2020, Felix Tshisekedi aliunda muungano wake mpya wa vyama vilivyopo karibu na utawala ''Union Sacre.''

Felix Tshisekedi anasimama kwenye uchaguzi huu wa urais wa mwezi Disemba akiongoza muungano huo wa ''Union Sacree'' wenye vyama zaidi ya 500 katika nchi nzima.

Kati ya washirika wake wakuu ni pamoja na mbabe wa zamani wa kivita Jean Pierre BEMBA wa chama cha MLC ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Mkuu pamoja na Vital Kamerhe, Waziri wa Fedha na kiongozi wa Chama cha UNC. Lakini pia Spika wa Seneti Bahati Lukwebo pamoja na Spika wa Bunge Mboso Nkodia ambao wote wanawakilisha vyama vyao katika muungano huo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Felix Tshisekedi wa DRC. 

Kampeni yake Tshisekedi tangu tarehe 20 Novemba imejikita kwenye muendelezo wa mageuzi aliyoyaanzisha mwaka 2018.

''Nipeni miaka mingine mitano niendeleze mipango yangu na kuifanya Congo nchi iliyoendelea yenye hadhi sawa na utajiri wake,'' amesikika akisema mara kwa mara.

Kati ya mambo mengi, Tshisekedi pia ameahidi kuifanya elimu ya sekondari kuwa ya bure baada ya elimu ya msingi kuingizwa katika mpango wa bure miaka mitano iliopita. Lakini pia kueneza kuboresha huduma ya afya na kuwa bure hasa kwa kina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Aidha Tshisekedi ameahidi kuiangalia upya mikataba ya madini ili kutunisha hazina ya Congo na kuwezesha ujenzi zaidi wa miundombinu.

Felix Tshisekedi amesema iwapo atapewa ridhaa na wananchi ya muhula wa pilia, basi atairudishia DRC hadhi na uhuru wake. Wakati huo huo, amenadi azma yake ya ya kufyeka makundi yote ya waasi Mashariki mwa Congo ikiwemo Kikundi cha M23.

''Kazi ya kumshinda adui imesalia ndogo. Naomba mniamini. Nipeni muhula mwengine. Nitalikomboa eneo lote la Mashariki,'' amesema.

Felix Tshisekedi.

Kwenye kampeni yake ya uchaguzi Felix Tchisekedi anaamini kuwa ushindi wake haupingiki.

''Nawaomba raia amkeni mapema tarehe 20 Disemba kupiga kura, tumalize kazi mapema. Ushindi kwa vyovyote ni wetu. Tuliyoyafanya miaka mitano ya nyuma ni dhahiri. Tunastahili kushinda ili tuendeleze miradi ya kuijenga Congo.''

Wadadisi wa siasa za Congo wanahisi kuwepo kwa wagombea wengi wa upinzani inaweza kumsaidia Felix Tshisekedi kuibuka mshindi.

Ithiel Batumike ni mtafiti katika Taasisi ya EBULELI ya Utawala Bora nchini Congo anasema, ''Kwa vile wapinzani hadi sasa wameshindwa kuafikiana kuhusu mgombea mmoja licha ya kukutana nchini Afrika ya Kusini, hali hii ni kama inamsaidia Tchisekedi. Na katika uchaguzi huu wenye duru moja pekee, inaweza kumsaidia kushinda uchaguzi.''

Raia wanaokadiriwa milioni 44 ndio watapiga kura tarehe 20 Disemba katika uchaguzi wa urais wenye wagombea 23, lakini pia uchaguzi wa wabunge wa kitaifa, wabunge wa majimbo pamoja na wakuu wa mikoa.

Tshisekedi alitoa dola milioni 200 kwa ajili ya malipo ya ziada katika DRC. Picha : Ikulu DRC.

Denise Nyakuru mwenye asili ya mji wa Bukavu ni mke wa rais Tshisekedi ambae wamejaaliwa watoto watano. Wanne wa kike ambao ni Fanny, Christina, Sabrina na Serena. Antony ndio mtoto pekee wa kiume wa rais Tshisekedi.

Maisha ya ukimbizi

Felix Tshisekedi alipata elimu ya msingi na sekondari mjini Kinshasa licha ya kukatizwa shule akiwa na umri wa miaka19 kutokana na misukosuko ya kisiasa iliyomsibu mzazi wake.

Baba yake ÉtienneTshisekedi wa Mulumba hatimae mwaka 1982 aliunda chama cha 'Union Pour la Démocratie et le Progrès Social' (UDPS), chama cha Upinzani dhidi ya Rais Mubutu Sese Seko akiwa madarakani.

Harakati za kisiasa za Tshisekedi 'Baba' zilimsababishia kuwekwa mara nyingi korokoroni na familia kulazimika kuhama Kinshasa nakwenda kujificha katika kijiji chao cha asili katika eneo la Kassai. Hata hivyo, hiyo haikuwa dawa. masaibu yaliendelea kuwaandama.

Akiwa na umri wa miaka 22, Felix Tshisekedi alikwenda uhamishoni akiwa na mama yake na ndugu zake na kupata hifadhi mjini Brussels, Ubelgiji. Na hapo Ndipo alipokea jina lake la Utani la ''Fatshi'' ambalo anafahamika nalo hadi leo.

President Felix Tshisekedi - Ikulu ya DRC

Felix 'akajiunga' kwenye Chuo Kikuu na kusomea katika Kitivo cha Masoko na Mawasiliano. Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wake wanahoji uhalisia wa shahada yake.

Safari ya kisiasa

Nchini Ubelgiji, Felix Tshisekedi alipambana dhidi ya utawala wa Kinshasa. Hatua kwa hatua alijiimarisha katika Chama cha 'Baba' cha UDPS (Union pour la Démocratie et le Progrès Social) na kuchukua nyadhifa mbalimbali. Kwanza kama Katibu wa kitaifa wa chama Ugenini, kisha Naibu Katibu Mkuu hadi kuchukua uongozi.

Mwaka 2011, Étienne Tshisekedi alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mbuji-Mayi katika eneo la Kassai. Mwaka huo, Baba yake Étienne alishindwa uchaguzi na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.

Mzee Étienne Tshisekedi alifariki dunia tarehe mosi Februari 2017 nchini Ubelgiji. Na kuzikwa miaka 2 baada ya kifo chake.

Mtoto wa baba arithi chama

Baada ya kifo cha baba yake, safari ya kisiasa ya Felix Tshisekedi ilikwenda kwa kasi.

Kufuatia makubaliano ya mwaka 2017 kati ya serikali na upinzani maarufu ''Accords de Saint Sylvestre,'' jina lake lilitajwa kuwa na uwezekano wa kushililia wadhifa wa Waziri Mkuu, lakini hatimae Joseph Kabila akamchagua Bruno Tshibala.

Lakini Felix Tshisekedi hakuvunjika moyo. Aliendeleza harakati zake za kisiasa na kuchukua uongozi kamili wa chama cha UDPS hadi kuwa mgombea wa Chama katika Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2018. Alishinda uchaguzi wa urais kwa kunyakuwa asilimia 36 ya kura na kutawazwa tarehe10 Januari 2019 kama Rais wa tano wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na rais wa kwanza kupokea kijiti cha mamlaka katika njia za kikatiba na amani tangu Congo iliponyakuwa uhuru wake mwaka 1961.

Cha Kufahamu:

-Sehemu kubwa ya maisha yake, Felix Tshisekedi aliishi nchini Ubelgiji mbali na nchi yake DRC.

-Ni mtoto aliyepata mafanikio kupitia kivuli cha baba yake Étienne.

-Ngome yake kubwa ya uchaguzi ni katika majimbo ya Kinshassa, Kassai Na Bas-Congo ikiwa ni maeneo ya Magharibi mwa DRC.

-Burudani ya F. Tchisekedi ni muziki wa nyumbani Rhumba lakini pia ni mpenzi mkubwa wa Kandanda. Na timu anayoishabikia zaidi ni Paris Saint Germain PSG ya France na nyota wake Kylian MBAPPE.

TRT Afrika