Ethiopia yasema oparesheni ya kuwarejesha raia wake kutoka Saudi Arabia imekamilika

Ethiopia yasema oparesheni ya kuwarejesha raia wake kutoka Saudi Arabia imekamilika

Makubaliano yalifanywa kati ya Serikali za Ethiopia na Ufalme wa Saudi Arabia kuwarejesha wahamiaji haramu
Serikali ya Ethiopia inasema imekamilisha oparesheni ya kuwarudisha raia wake nyumbani kutoka Saudi Arabia  / Photo: AP

Harakati mpya ya Ethiopia kuwarudisha wananchi wake kutoka Saudi Arabia ilianza Machi 2022 kwa lengo la kuwarudisha raia wake 100,000. Wote hawa walienda Saudi Arabia kwa njia isiyo halali.

Tume ya kudhibiti hatari ya maafa ya Ethiopia, inasema hadi sasa imesaidia raia 131,642 kurejea nyumbani kutoka nchi ya Mashariki ya Kati.

Mwaka 2022 Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, lilikadiria kuwa takriban Waethiopia 750,000 waliishi Saudi Arabia huku takribani 450,000 kati yao walisafiri kwenda nchini humo kwa njia zisizo za kawaida.

IOM inasema uhamiaji kupitia njia ya Mashariki inayoanzia pembe ya Afrika hadi Saudi Arabia mara nyingi unatokana na njia zisizo za kawaida.

Ethiopia baada ya muda imekuwa ikilaumu walanguzi wa binadamu kwa kujinufaisha kwa raia wanaotafuta mapato bora.

TRT Afrika