EWURA imevifungia vituo saba vya kuuza mafuta vilivyothibitika kuficha mafuta kinyume na kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini

Na Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania – EWURA, imevifungia vituo saba vya kuuza mafuta vilivyothibitika kuficha mafuta kinyume na kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini.

Mamlaka hiyo ilisema baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo kwa makusudi waliamua kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi ya kibiashara ikiwemo faida kubwa kutokana na ongezeko la bei.

“Wamiliki wa vituo vya mafuta kwa makusudi kabisa waliamua kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi ya kibiashara kutokana na ongezeko la bei za mafuta kinyume na sharia, kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini,”

Titus Kaguo, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano, EWURA

Katika taarifa ya Mamlaka hiyo kwa vyombo vya habari jijini Dodoma kuwa pamoja na mafuta kuwepo nchini lakini changamoto ya upungufu katika baadhi ya maeneo ya nchi ilichangiwa kwa kuficha mafuta.

“Wamiliki wa vituo vya mafuta kwa makusudi kabisa waliamua kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi ya kibiashara kutokana na ongezeko la bei za mafuta kinyume na sharia, kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini,” Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo alisema.

Pamoja na hatua hizo za kuvifungia vituo hivyo, lakini vilipewa fursa ya kuwasilisha utetezi wao ndani ya siku 21. Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa idadi ya vituo vilivyofungwa.

“Baada ya utetezi wao EWURA ilijiridhisha kuwa vituo vilitenda kosa kati ya mwezi wa saba na mwezi wa nane hivyo kuamua kuvifungia kwa miezi 6,” alisema. Pamoja na hayo imekiri kuwa mafuta yaliopo kwa sasa yanajitosheleza nchini.

Miezi kadhaa nyuma kumekuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ongezeko la bei ya mafuta katika maeneo mbalimbali ikiwemo makao makuu ya nchi Dodoma.

Vita vya Urusi na Ukraine pia vimechangia kwa kiasi kikubwa kudorora kwa usafirishaji wa mafuta. Urusi pekee ina takriban 500 kati ya 1000 zinazosafirisha mafuta katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

TRT Afrika