Mwaka  wa 2022 zaidi ya watu 3800 walipoteza maisha kwenye ajali za barabarani nchini Kenya.  / Photo: Reuters

Na Kevin Momanyi

Iwapo wabunge watakubali Mswada huo mpya, Kenya inatarajia kutumia angalau dola bilioni1.5 kila mwaka katika barabara zote za umma kwa kujenga huduma za usafiri zisizo za magari (NMT) kama vile njia za kutembea na njia za baiskeli.

Mswada huo unalenga kurekebisha Sheria ya Barabara ya Kenya ya 2007 ili barabara zote za umma nchini, iwe za mijini au mashambani, lazima ziwe na njia zilizotengwa kutumiwa na wasio na magari.

Kulingana na takwimu kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama ya Kenya ajali za barabarani huenda zikapunguka maradufu ikiwa mswada huu utapitishwa.

Mwaka jana, zaidi ya watu 3800 walipoteza maisha kwenye ajali za barabarani nchini Kenya. Kenya ina takriban kilomita 22000 za barabara za lami, ambazo ni takriban kilomita 3000 pekee ndizo zinazozingatia mahitaji haya ya sheria.

"Gharama ya kutoa huduma zisizo za magari katika pande zote mbili za barabara ni takriban KSh milioni 10 kwa kilomita kulingana na makadirio ya wahandisi wa Mamlaka ya Barabara za Mijini (KURA)," Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda aliyefadhili mswada huo alisema.

Kwa kuunda njia hizi za kutembea na baiskeli, watembea kwa miguu na waendesha baiskeli watakuwa na njia zao hivyo basi kuboresha usalama wao na kupunguza ajali za barabarani. Mradi huu wa ujenzi unatarajiwa kuwa wa kilomita 116 kote nchini.

Haya ni maendeleo yenye matumaini kwa taifa hili la Afrika Mashariki kwa sababu kuongeza njia za baiskeli kwenye barabara za magari kutapunguza uwezekano wa ajali na uchafuzi wa mazingira kutokana na magari ambayo waendeshaji wangeweza kutumia.

TRT Afrika