Njia hii imetumika na akina mama wa Amboseli kama sehemu ya Uhifadhi. / Picha: WWF-Kenya  

Na Sylvia Chebet

Wakati dunia ikiadhimisha 'saa ya dunia', na majengo mengi maarufu yakizima taa kwa saa moja siku ya Machi 23, akina mama wa Amboseli waliozungukwa na nyika waliazimia kuadhimisha saa hiyo kwa kufanya jambo la kipekee zaidi.

Walichimba mamia ya 'nusu mwezi' yenye kufanana na nyuso zenye kutabasamu, ndani ya Hifadhi ya Amboseli inayopatikana chini ya Mlima Kilimanjaro.

Kingo hizi ndogo za ardhini hutumika kwa shughuli muhimu, kukusanya maji ya mvua yanayotiririka ambayo yangesomba ardhi kavu, isiyo na maji, na kusababisha mmomonyoko wa ardhi na mafuriko.

"Tumeshashuhudia mabadiliko mengi, tumeona nyasi zikichipuka na kwa kweli inawatia moyo watu wanaofanya kazi hiyo, wanaona matokeo mara moja," meneja wa Big Life Foundation anayesimamia mradi huo, Ernest Lenkoina anaiambia TRT Afrika.

Mwanajamii anayeishi karibu na hifadhi hiyo, Ngameri Maiyo anakubaliana na kauli hiyo.

"Ng'ombe wetu wanapata majani ya kutihzetu zimepata nyasi, na wanyama pori wa aina mbalimbali sasa wameletwa hapa; pundamilia, swara, hata simba siku hizi wanakuja kusubiri swala huko kwa sababu kumekuwa na majani mengi. Tumefanya vizuri sana," anasema.

“Tulipata shida sana mashambani. Hata hawa swala ukipanda maharage, wanakula, lazima upande zao lingine kabisa. Mradi huu umenifurahisha,” Ngameri aliongeza.

Eneo hilo la Uhifadhi ni sehemu muhimu kwa wanyamapori kutawanyika hasa wanapokuwa wakiingia kwenye hifadhi za Amboseli na Tsavo. Pia ni muhimu sana kwa maisha ya jamii ya Wamasai, wanaitumia kwa kiasi kikubwa kwa malisho ya mifugo.

Nyumbu ndani ya hifadhi hiyo wakivuka katika shoroba ya Amboseli na Tasavo /Picha: WWF-Kenya

Tabasamu la Dunia

'Vijimwezi hivi' huwa na urefu wa mita 2.5 na upana wa mita 5, likikaribia ukubwa wa tembo mdogo.

Zikiwa zimewekwa kwenye miteremko huku upande 'uliofungwa' ukitazama chini, vifurushi hivi hunasa kwa ufanisi na kupunguza kasi ya kutiririka kwa maji.

Matokeo yake, sio tu hukusanya maji ya mvua, lakini pia huruhusu kunyonya kwenye udongo na uhifadhi kati ya vipeto.

Miundo hii ya udongo yenye nusu duara, iliyoundwa kuhifadhi maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo, imethibitisha ufanisi katika kuimarisha rutuba ya udongo, na kurekebisha ardhi iliyoharibiwa, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.

"Na kwa sababu vipeto vinafanywa kwa kiwango kikubwa, basi vinazidi kuenea hadi eneo lote lilofunikwa na uoto wa kijani," Samuel Jakinda, meneja wa programu ya 'Just Dig It' anaongeza, akibainisha kuwa hii inaathiri kwa kiasi kikubwa viumbe hai, asilimali, watu, na hali ya hewa.

Akina mama hao walijitoa kikamilifu kwa ajili ya siku hiyo. Picha: WWF-Kenya

"Tunatumia vifurushi hivyo kama njia ya kukabiliana na hali ya hewa kwa sababu eneo hilo limeharibiwa sana na uharibifu huo unatokana kwa kiasi kikubwa na mfumo wa malisho ya kienyeji kuporomoka. Dk. John Kioko, mratibu wa programu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF-K) katika mandhari ya Amboseli Chyulu.

"Na kwa hivyo, tunahitaji kurudisha uhai wa mfumo wa ikolojia na jinsi bendi inavyosaidia kufanya kazi kama sehemu ndogo ya maji, na inazuia udongo," aliongeza.

Mradi huo unaoendeshwa na WWF-K, Just Dig It, na Big Life and Big Life Foundation, ulianza mwaka wa 2021 katika jitihada za kuimarisha ustahimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa miongoni mwa jamii katika nyanda za malisho.

"Hadi sasa, tumerejesha hekta 10,000 kupitia hatua tofauti za tulizozichukua na tunachotambua ni kwamba tangu 2021 kuna matokeo ya ushahidi na haya ni pamoja na uboreshaji wa hifadhi katika baadhi ya tovuti hizi," Kioko wa WWF-K anasema.

Jamii ya eneo hilo imeshuhudia ongezeko la viumbe hai katika ardhi yao ikiwa ni pamoja na wadudu wapya, ndege na wanyama na hata mimea mipya. Hii imewapa msukumo wanawake kuendelea kuchimba vipeto.

"Kwetu sisi tumekuwa tukifanya Saa ya Dunia kila siku. Kila siku asubuhi, tunakuja hapa na kufanya kazi kwenye Saa ya Dunia. Saa ya Dunia inapaswa kuwa inaendelea. Binafsi nachimba mitaro sita kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa mbili usiku. Ikiwa sisi wanawake wote 120 tutachimba mafungu sita kila moja kwa siku, hiyo ni vipeto vyingi," Valentine Semeya anasema

"Tushirikiane, tuunganishe nguvu na tuharakishe ustawishaji wa maeneo yaliyoharibiwa." Jakinda anaongeza.

Wanawake wa jamii hiyo wakiandaa 'nusu mwezi ardhini'./Picha: 

"Viongozi wa mpango huo kwa kweli ni wanawake. Na ilikuwa ni kwa kubuni kwa sababu tuligundua kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri zaidi wanawake ingawa hawaji mitaani na kulalamika."

Sketa Imelaisa, mwanajamii wa hifadhi hiyo anaamini kuwa mradi huo utakuwa na matokeo chanya.

"Wakati mwingine ukame unatushinda, tuna mifugo na hakuna mahali pa kulisha, lakini miaka ijayo tunaona nyasi hizi zitatusaidia sisi Wamasai," Imelaisa anasema.

"Wakati wa kiangazi, tulikuwa tunanunua nyasi. Ikiwa huna pesa, unaweza hata kuhisi kushawishika kuiba kwa sababu unahitaji nyasi kulisha ng'ombe wako, lakini huna uwezo wa kumudu," Purity Seya anaongeza kusema.

"Ng'ombe wakija hapa watashiba, na sisi tutapata maziwa ili kusaidia maisha ya watoto wetu. Pia tutapata pesa za kusaidia vikundi vyetu, na watoto wetu wataweza kwenda shule."

TRT Afrika