Serikali ya Kenya imeipa kampuni ya Adani kutoka India kandarasi ya ujenzi wa njia hizo kupitia Mpango wa Miradi ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi, kulingana na mshauri wa Rais wa mambo ya uchumi.
Mpango huo unategemea kugharimu kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1.3, amesema David Ndii kwenye ukurasa wake wa X.
"Serikali kupitia KETRACO imeipa kampuni ya Adani na Africa50 mradi wa kujenga njia za kusafirisha umeme," aliandika Ndii. "Gharama za mradi huo ni kiasi cha dola za kimarekani 1.3 bilioni."
Africa50 ni kampuni tanzu ya Benki ya Maendeleo ya Afrika inayojishughulisha na maendeleo ya miundombinu.
Mradi wa Uwanja ndege
Mbali na mradi huo tarajiwa, serikali ya Kenya pia imeipa tenda ya kuukodisha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa kampuni ya Adani Group.
Mradi huo unahusisha ukodishwaji wa uwanja huo kwa kampuni hiyo kutoka India kwa kipindi cha miaka 30.
Kampuni ya Adani inaendesha viwanja saba vya ndege nchini India na kwa muda mrefu sasa, imekuwa ikikosolewa na vyama vya upinzani nchini humo kwa madai ya kupendelewa na serikali.