Sokwe mtu wana asili ya upole na huonyesha tabia na hisia nyingi kama zile za binadamu, ikiwemo hisia za furaha na huzuni / Picha: AP

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Afrika hatimae ina habari njema, nayo ni kuongezeka kwa idadi ya sokwe mtu. Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, kumekuwa na idadi ya sokwe mtu wa milimani 680, lakini sasa hivi idadi hiyo inaonekana kuongezeka na kufikia zaidi ya sokwe mtu 1000.

Sokwe mtu wana asili ya upole na huonyesha tabia na hisia nyingi kama zile za binadamu, ikiwemo hisia za furaha na huzuni.

Kwa kweli, sokwe mtu hushiriki asilimia 98.3 ya kanuni zao za kijeni na wanadamu, hivyo kuwafanya kuwa binamu wa karibu baada ya sokwe wengine na bonobos.

Viumbe hawa, wanaishi hasa katika misitu iliyo juu ya milima, kwenye miiinuko ya futi 8,000 hadi 13,000.

Wana manyoya mazito ikilinganishwa na nyani wengine wakubwa. Manyoya huwasaidia kuishi katika makazi ambayo hali joto mara nyingi hupungua chini ya barafu.

Wengi wa sokwe mtu hawa wanaishi katika Milima ya Virunga ambayo inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Uganda. Wengine wanapatikana katika Mbuga ya Kitaifa ya Bwindi nchini Uganda.

Jike anaweza kuzaa mtoto mmoja tu kila baada ya miaka minne hadi sita na watatu au wanne tu katika maisha yake yote / Picha: AP 

Sokwe mtu huishi katika vikundi vya familia vya wanyama 5 hadi 10, lakini wakati mwengine kuanzia 2 mpaka zaidi ya 50, wakiongozwa na dume aliyekomaa ambaye hushikilia cheo chake kwa miaka mingi.

Sokwe huyu wa kiume ana uzito wa zaidi ya kilo 180 ambazo zinachangiwa na yeye kula takriban kilo 18 kila siku za majani, mashina ya miti na matunda.

Jike anaweza kuzaa mtoto mmoja tu kila baada ya miaka minne hadi sita na watatu au wanne tu katika maisha yake yote. Kiwango hiki cha chini cha uzazi kinafanya iwe vigumu kwao kupona kutokana na kupungua kwa idadi ya watu.

Lakini wanyama hawa, ambao ni fahari ya Afrika wamekuwa na changamoto ya kuadimika. Kwa muda mrefu, wametishiwa na ujangili, magonjwa na ukataji miti.

Pia wameangamizwa kwa sababu ya maambukizi ya magonjwa kutoka kwa binadamu, na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo, habari njema ya iaddi yao kuongeza imepokelewa kama maendeleo makubwa na mashirika ya wanyama kama WWF.

Sokwe mtu huishi katika vikundi vya familia ya wanyama 5 hadi 10, lakini wakati mwengine kuanzia 2 mpaka zaidi ya 50/ picha: AP 

Wataalamu wanasema kuongezeka kwao kumechangiwa na mikakati bora ya uhifadhi - ambayo ni pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara na uangalizi wa wanyama hao, matibabu ya magonjwa ya kupumua, na kuondolewa kwa mitego iliyowekwa kwa wanyama wengine wadogo ambayo hushambulia sokwe mtu wachanga imesaidia idadi yao kuongezeka.

Jamii katika maeneo ya msitu pia wanaendelea kuhamasishwa na kusaidia kutunza mazingira ya wanyama hao. Kulipia kuwaona sokwe mtu kupitia Uganda au Rwanda inagharimu kati ya dola 450 na 1500, ikiwa fedha hizi zinachangia katika utalii.

Fedha hizi zinachangia katika uhifadhi wa makazi ya wanyama hawa. Wataalamu sasa wanasema hivi sasa Rwanda, DRC na Uganda zina jukumu la kuhakikisha kuwa mikakati mizuri ya kuwatunza inaendelea kutimizwa ili idadi ya sokwe mtu iendelee kuongezeka.

TRT Afrika