Kutana na ‘mama’ wa watoto waliopoteza wazazi wao kutokana vita nchini Kongo

Kutana na ‘mama’ wa watoto waliopoteza wazazi wao kutokana vita nchini Kongo

Marie Mutsuva aliamua kubaki mpweke baada ya kugundulika kuwa na hali ya kiafya iliyomzuia kushika mimba.
Hail Marie

Huyu ni Marie Mutsuva ambae aliamua kutoolewa baada ya vipimo kuonyesha kuwa ana tatizo la kiafya ambalo lingemzuia kupata mtoto.

Miongo kadhaa baadae, Mutsuva, amekuwa mama kwa watoto yatima kadhaa ambao wamepoteza wazazi wao kutokana na vita vya muda mrefu ambavyo vimesambaratisha eneo la mashariki ya DR Kongo.

Tangu mwaka 2014, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema, zaidi ya watu 4,000 wameuawa na makundi ya waasi yajulikanayo kama Allied Democratic Force (ADF), ambalo linajulikana kama tawi la kundi la kigaidi la Daesh la Afrika ya Kati.

Kwa watoto ambao wazazi wao wameuliwa katika machafuko hayo, Marie Mutsuva amekuwa ndio mlezi wao. Na nyumba yake iliyopo katika mji wa Beni ndio sehemu yao ya furaha.

“Ni miaka 43 sasa tangu nimeanza kuwasaidia watoto yatima baada ya kuambia kwamba sitaweza kuzaa,” Mutsuva ameiambia TRT Afrika.

“Kwa sasa hivi, nina watoto 58 katika kituo changu cha kulea watoto yatima na wengi wao wanatoka maeneo ambayo waasi wa ADF wameuwa familia zao.”

Mapambano ya kila siku

Mutsuva anaamka kila siku saa kumi na moja alfajiri ili kuwaandalia watoto chakula, ambao wana umri kati ya miazi tisa hadi miaka 18. Anaendesha kituo hicho kupitia michango ya fedha na vifaa, kutoka kwa wasamaria mwema.

Tuna shida ya kupata chakula, matibabu, na ada ya shule lakini pia mahali pa kulala.Hata kama sijapata watoto, watoto hawa yatima wananiita MAMAN... MAMAN...MAMAN, ninahisi furaha na najihisi kuwa nina mzigo mzito zaidi kuliko wanawake ambao wamepata watoto, "anasema Bi Mutsuva.

Ingawa anapambana kuwapa mahitaji yao ya kila siku, lakini anasema furaha yake kubwa ni pale anaposikia wakimuita “mama, mama… kila siku” hii inafidia jasho lake.

“Tuna tatizo la upatikanaji wa chakula, huduma ya matibabu, ada ya shule, na hata kupata sehemu nzuri ya malazi,” amesema.

Kwa watu wengi wanaoishi jirani na kituo cha watoto yatima cha Marie Mutsuva, wanamchukulia kuwa mwanamke shujaa na wanataka kuona serikali ya Kongo na watu wenye moyo mwema wakuje kumsaidia kulisha, kusomesha na kulipia matibabu ya watoto hao.

“Kituo hicho cha kulea watoto yatima kina uwezo wa kuchukua watoto 20 pekee, lakini hivi sasa tuna watoto 58…na idadi inaweza kuongezeka iwapo machafuko yataendelea.”

Mutsuva amejaribu kutafuta ndugu na familia za watoto anaowalea, lakini zoezi hilo limekuwa gumu kwake.

Mara moja kwa mwezi, anaalikwa na moja ya vituo vya redio ambapo hutoa majina na taarifa nyengine za watoto anaowalea.

Mara ya mwisho ambapo mtoto mmoja aliungana na familia yake ilikuwa ni mwezi Septemba, mwaka 2017.

“nilipata binti wa miaka mitatu kutoka Eringeti, kama kilomita 60 kutoka Beni,” Mutsuva anakumbuka. Wiki moja baadae, alipomzungumzia katika kipindi cha redio, “shangazi wa mtoto alinipigia simu, na mtoto aliungana na familia yake.”

Hata hivyo, watoto hawana shauku kubwa ya kuungana na familia zao, kwa sababu wapo chini ya uangalizi mzuri wa Mutsuva.

“Nahisi ujasiri… kwa sababu naweza kuendelea na masomo, shukrani kwa mama yangu Marie Mutsuva,” Glory Somana, 14, anaiambia TRT Afrika.

“Hii ndio familia yangu…watoto wote waliopo hapa nawaona ni kaka zangu na dada zangu. Nitakapomaliza masomo yangu, nitamsaidia Mama Marie kulea watoto wengine yatima,” anasema binti huyo.

Shujaa kwa wote

Kwa wanaomjua Mutsuva, wanamuona ni shujaa wa nguvu asiye na kofia. Na ni matumaini yao kwamba serikali ya Kongo itakuja kumsaidia kulisha, kulipia ada na kutoa huduma za matibabu kwa watoto.

“Kwangu mimi, inaniwia taabu kulisha watu wachache wa familia yangu, lakini yeye analisha watoto 58..Mungu ampe umri mrefu ili atimize ndoto yake,” anasema Muhindo Nzala, jirani wa Mutsuva.

Huo pia umekua ni mtazamo wa Kapteni Antony Mwalushayi, msemaji wa Jeshi la Kongo na sehemu ya Operesheni ya Sokola dhidi ya makundi yenye silaha mashariki mwa DR Kongo.

“Serikali ya Kongo sharti imsaidie Mama Marie kwa chakula na huduma ya matibabu kwa sababu ni mwanamke mwenye ujasiri anaetoa tumaini kwa watoto waliopoteza matumaini.

“Wanawake kama Marie Mutsuva, mimi nawaona kama malaika,” Kapteni Mwalushayi anaiambia TRT Afrika.

“Jeshi la Kongo linafanya kila liwezalo kutokomeza makundi haya ya waasi ili watu wa eneo hili wawezi kuishi kwa amani. watu ambao wanaathirika zaidi wakati wa vita ni wanawake na watoto ambao hawawezi kujiokoa panapotokea mashambulizi kama hayo.”

Mwezi Januari, tarehe 22, watoto watano wamekuwa miongoni mwa watu kumi waliouawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika kanisa la Pentecostal lililopo Kasindi mashariki mwa Kongo.

“Mashambulizi ya hivi karibuni ni dhahiri kwamba, mashariki mwa DRC ni eneo hatari kwa watoto,” anasema Grant Leaity, mwakilishi wa shirika la Umoja wa Matafia la UNICEF nchini DRC.

“Kwa mujibu wa madaktari, katika hospitali kuu ya Kasindi, angalau watoto 16 walijeruhiwa katika shambulio hilo, sita kati yao walipata majeraha mabaya zaidi.”

Ameongeza kwamba, angalau watoto 40 wametengwa na familia zao kutokana ma kuibuka kwa mashambulio ambayo yamesababisha watu kuhama makazi yao kutoka maeneo kama vile Djugu, Mahagi na Aru.

“Wakati tunalaani mashambulio yote dhidi ya raia, hatutasita kufanya kazi saa 24 kuwalinda wao na familia zao,” Leaity amesema.

TRT Afrika