Kuna watu ambao wanapenda kufuga mbwa kwa ajili ya starehe, wengine kwa ajili ya ulinzi na usalama. / Picha: Reuters

Coletta Wanjohi

TRT Afrika , Istanbul

Mbwa ni rafiki mtiifu kwa binadamu wakati wote.

Kuna watu ambao wanapenda kufuga mbwa kwa ajili ya starehe, wengine kwa ajili ya ulinzi na usalama.

Pia kuna mbwa ambao kazi yao ni kutoa huduma, wanaojulikana kama mbwa wa usaidizi.

Wanapewa mafunzo maalumu kurahisisha moja kwa moja changamoto zinazohusiana na mtu mwenye ulemavu wa kimwili, kiakili, au ukuaji.

German Shepherd ni mbwa wa kijerumani ambaye hutumiwa kama mbwa wa polisi/ picha kutoka Getty 

Lakini licha ya mbwa kuwa rafiki wa karibu wa mwanadamu, kwa nini, baadhi ya nyakati mbwa bado anaweza kubadilika na kuanza kumshambulia mmiliki wake?

Aina tofauti ya mbwa wakali

Hebu tuangalie tu aina chache ya mbwa wanaosemekana kuwa na uwezo wa kuwa wakali kwa sababu tofauti.

German Shepherd ni mbwa wa kijerumani ambaye hutumiwa kama mbwa wa polisi. Ni mbwa mwenye akili sana, anayeweza kufunzwa kwa urahisi na mwepesi wa kukimbia.

Akikuuma anaweza kukuvunja mifupa, hivyo haishangazi akifanya fujo anaweza kusababisha hatari halisi. Huskies wa Siberia kwa ujumla wanaweza kuonyesha tabia ya fujo kama matokeo ya mafunzo duni.

Mbwa hawa wanaweza kuwa wakaidi na kuleta changamoto hata kwa wamiliki wenye uzoefu wa mbwa.

Doberman Pinschers awali walikuzwa kama mbwa wa ulinzi na wametumiwa baadaye kama mbwa wanaofanya kazi polisi na jeshini.

Wataalamu wanasema kukosa kumzoesha au kumtambulisha mbwa katika jamii inayomzunguka, huenda ikamfanya akawa na tabia tofauti/ picha AP

Dobermans wanaweza kuwa na fujo kwa watu ambao hawawajui kwa hofu au kwa tamaa ya kulinda wamiliki wao.

Rottweilers nao wana sifa ya kuwa na fujo zaidi ya mbwa wengine.

Jack Russell Terriers nao ni mbwa ambao pindi wanapomzoea mtu mmoja au sehemu ya wanafamilia, huwa hawataki kumzoea mtu mwengine, wanawaangalia wamiliki wao kama milki yao au mali yao binafsi.

Wanaweza kuonyesha tabia ya ulinzi mkali.

Hawa ni baadhi tu ya wengine wengi wenye tabia za ukali kupita kiasi,

Mbwa kubadilisha tabia

Wataalamu wanasema kukosa kumzoesha au kumtambulisha mbwa katika jamii inayomzunguka, huenda ikamfanya akawa na tabia tofauti.

Wanasema mbwa ambao hawajaonyeshwa watu vya kutosha, wanyama na mazingira tofauti wakati wa kipindi chao muhimu yaani kati ya umri wa wiki 3 hadi 14 wanaweza kuwa na hofu au wasiwasi katika hali isiyojulikana.

Hofu hii wakati mwengine inaweza kusababisha athari za fujo, haswa wakati mbwa anahisi maisha yake au ya mmiliki wake kuwa hatarini.

Mbwa wengine ni wa starehe / Picha AFP 

Ukikosa kumpa mbwa wako mafunzo sahihi katika wakati sahihi, hii inaweza kugeuka kuwa changamoto kwako na familia yako. Hataelewa kinachotarajiwa kutoka kwake, na kusababisha kuchanganyikiwa.

Mazoezi ya kimsingi ya utii, kama vile kumfundisha kutii amri tofauti huweka msingi wa mawasiliano kati yake na mmiliki. Mbwa ni mnyama anayehitaji upendo, tahadhari, na kusisimuliwa kiakili.

Kwa hivyo, ukiyapuuza mahitaji haya, unaweza kusababisha mabadiliko yake ya kitabia.

Mbwa ambao wameachwa pekee yao kwa muda mrefu bila mazoezi au uboreshaji wa kiakili wanaweza kuchanganyikiwa na kupata wasiwasi, ambao unaweza kujidhihirisha kama tabia ya fujo.

Hofu na wasiwasi ni hisia za kawaida zinazopatikana kwa mbwa, na ikiwa hazijashughulikiwa, zinaweza kuongezeka na kusababisha uchokozi. Na hapo ndipo anapoweza kukushambulia akijaribu kulinda mali yake, kama vile chakula, vinyago, au hata sehemu anayopenda zaidi kupumzika.

Wakati mwingine, tabia ya fujo katika mbwa inaweza kuhusishwa na hali ya msingi ya matibabu. Magonjwa au majeraha fulani yanaweza kusababisha mbwa kupata maumivu au usumbufu, na kusababisha mabadiliko katika tabia yake.

Kwa hivyo, unapoamua kununua mbwa, kumbuka kuwa ni lazima kumuandaa na kumpa uzoefu wa kijamii na kuhakikisha yuko sawa wakati wote, kwa usalama wako, familia yako na jamii inayokuzunguka.

Pia ni muhimu sana kuhakikisha mbwa wako anapata chanjo zote zinazohitajika, mfano rabies, maarufu kama 'kichaa cha Mbwa'', ambayo inasemekana kuwa hatari kubwa zaidi kwani mtu akiumwa na mbwa na kuambukizwa Rabies, hakuna tiba.

TRT Afrika