Barghashi Abu msanii wa kizazi kipya nchini Tanzania. Picha/Barghashi.

Safari ya Abubakar Juma Amour, almaarufu "Barghash Abuu" katika tasnia ya mziki ilianza miaka 10 iliyopita. Kwanza alianza kuimba mashairi na ngonjera, na baadae ndipo alipojiingiza katika mziki wa kizazi kipya, Bongo Fleva.

Mbali na kuwepo kwa majina makubwa ya wasanii katika tasnia ya mziki wanaovuma nchini Tanzania, Afrika Mashariki na barani Afrika kwa ujumla, lakini bado wasanii chipukizi kama Barghash wanaonekana kutumia nguvu nyingi ili angalau kupenyeza kazi zao katika jamii inayowazunguka.

Akiongea na TRT Afrika, Barghash anasema safari yake haikuwa rahisi mpaka kuweza kurekodi nyimbo studio. "Nilianza kuimba mashairi na ngonjera kwenye maharusi na shughuli mbali mbali," anasema.

Barghashi Abuu kama ilivyo kwa wasanii wengine, na yeye pia anatumia mziki kuelimisha jamii. Picha/Barghashi. 

Kwa mujibu wa Barghash, wazazi wake hawakuonesha kuridhishwa na chaguo lake la kuwa mwimbaji, ingawa baada ya vute nikuvute walimruhusu.

’‘Mama alikuwa hataki kabisa niwe mwimbaji. Nikafikiria na hatimae nikatunga wimbo wa 'Forgive me Mama," anasema Barghashi.

"Na hapo, kabla ya mama kufariki akaniruhusu kuimba, nami nikaingia rasmi kwenye muziki kwa ari na nguvu zote," Barghash aliongeza.

‘’Natumia mziki kuelimisha jamii, ili iweze kuelimika na kustaarabika,’’ Barghash Abuu, anasema.

Barghash mpaka sasa tayari ashatoa nyimbo zaidi ya 10 na bado anaendelea na utunzi licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa maeneo ya kufanya video zake.

"Mama alikuwa hataki niwe mwimbaji, nikafikiria na hatimae nikatunga wimbo wa 'Forgive me Mama."

Barghashi Abuu, msanii wa Bongo Fleva, Dar es Salaam, Tanzania

Mbali na hilo, lakini pia kuna ugumu wa kupenyeza kazi zake na hatimae kuweza kujulikana kama ilivyo kwa wasanii wengine. Hiyo imemfanya Barghash kutoa wito kwa wasanii wakubwa na kuwakumbusha kuwashika mkono wale wanaochipukia.

Barghashi Abuu anasema, kwa sasa chanzo chake kikubwa cha mapato, ni kuimba katika shughuli mbalimbali ikiwemo maharusi.

"Licha ya uwekezaji nilioufanya kwenye maeneo ya dijitali lakini bado haujaanza kunilipa," anasema.

TRT Afrika