Jenerali  Francis Ogolla aliteuliwa kama Mkuu wa Majeshi wa Kenya mwezi Aprili 2023/ Picha: TRT Afrika    

Na Brian Okoth

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya Jenerali Francis Ogolla amefariki dunia, Rais William Ruto amethibitisha.

"Nimesikitishwa sana na kifo cha Jenerali Francis Omondi Ogolla, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya," alisema Ruto siku ya Alhamisi jioni, huku akitangaza siku tatu za maombolezo.

Ogolla alikuwa kati ya abiria 11 waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo ambayo ilishika moto baada ya ajali hiyo katika eneo la Sindar, kwenye mpaka wa kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi, majira ya saa nane mchana.

Watu tisa walifariki papo hapo, huku wawili wakijeruhiwa vibaya na kuwahishwa jijini Nairobi kwa matibabu zaidi. Maafisa hao wakuu wa kijeshi, ambao waliondoka katika mji mkuu wa Nairobi siku ya Alhamisi asubuhi, walikuwa kaskazini-magharibi mwa Kenya kwa majukumu ya kiofisi.

Rais Ruto alimteua Ogolla kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mnamo Aprili 28, 2023, akichukua nafasi ya Robert Kibochi, aliyetimiza umri wa kustaafu.

Kujiunga na Majeshi ya Ulinzi mwaka 1984

Siku hiyo, Rais alimpandisha cheo Ogolla, ambaye alikuwa Luteni-Jenerali na Makamu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), hadi cheo cha Ujenerali.

Kuapishwa kwa Ogolla kulifanyika Aprili 29, 2023 katika Ikulu ya Nairobi.

Ogolla alijiunga na Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Kenya tarehe 24 Aprili, 1984 na kupata cheo cha Luteni Usu, Mei 6, 1985 na kuhamishiwa katika Jeshi la Anga la Kenya.

Alipata mafunzo ya urubani na baadaye kama rubani mwalimu katika Jeshi la Anga la Kenya.

Umahiri katika akili ya picha

Tovuti ya wizara ya ulinzi ya Kenya inasema Ogolla pia alipata mafunzo katika nyanja zingine kama vile upelelezi wa picha, kukabiliana na ugaidi na uchunguzi wa ajali.

Jenerali huyo alikuwa mhitimu wa shule ya Kijeshi ya Paris huko Ufaransa na Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya.

Ogolla alipanda vyeo mbalimbali vya uongozi wa kijeshi wa Kenya, na akapandishwa cheo hadi meja jenerali na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, na baadaye akamteua Kamanda wa Jeshi la Anga la Kenya Julai 15, 2018.

Nafasi za uandamizi

Ogolla pia alishikilia nyadhifa za juu katika mafunzo, kamandi na wafanyakazi ndani ya mfumo wa kijeshi.

Hapo awali aliwahi kuwa naibu kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya, kamanda wa kikosi cha anga cha Laikipia, afisa mkuu wa mapigano ya anga , mwalimu mkuu wa urubani katika Shule ya Mafunzo ya Usafiri wa Anga ya Kenya, na afisa wa dawati la oparesheni katika Makao Makuu ya Jeshi la Anga la Kenya.

"Pia alihudumu katika iliyokuwa Yugoslavia kama mwangalizi na afisa habari wa kijeshi kutoka 1992 hadi 1993, kama mwenyekiti wa Military Christian Fellowship kutoka 1994 hadi 2004 na mwenyekiti mwenza wa Association of African Air Chief kutoka 2018 hadi 2019," wizara ya ulinzi ya Kenya inasema.

Ogolla ameacha mjane, Aileen Ogolla, na watoto wawili na mjukuu mmoja. Enzi za uhai wake, alipendelea kucheza gofu na kusoma vitabu.

Utata wa uchaguzi wa urais wa 2022

Mnamo Mei 2023, Rais Ruto alisema katika mahojiano kwenye televisheni ya taifa kwamba alimteua Ogolla Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi licha ya Ogolla kudaiwa kujaribu "kupindua" ushindi wake katika uchaguzi.

Rais Ruto alikuwa akichuana na mwanasiasa mkongwe Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022, na akashinda kwa tofauti ndogo.

Ruto, ambaye alihudumu kama Makamu wa Rais katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kutoka 2013 hadi 2022, na kupata kura milioni 7.18 (asilimia 50.5) dhidi ya kura milioni 6.94 za Odinga (asilimia 48.9) kushinda kinyang'anyiro cha urais.

Odinga alikuwa ameidhinishwa na Kenyatta, na aliposhindwa katika uchaguzi huo, ilidaiwa kuwa viongozi wakuu, akiwemo Ogolla, walijaribu kulazimisha bodi ya uchaguzi kuitisha uchaguzi huo kumpendelea Odinga, au kulazimisha urudiwe.

'Mtu sahihi kuongoza Jeshi'

Nchini Kenya, mgombea urais anahitaji kupata angalau asilimia 50 pamoja na kura moja ili kushinda uchaguzi katika duru ya kwanza, ambapo kushindwa, marudio ya wagombea wawili wa juu hufanyika.

Ruto alisema licha ya Ogolla kuwa sehemu ya timu “dhidi” ya ushindi wake, yeye (Ruto) alimteua Ogolla Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa sababu “Ogolla alikuwa mtu bora zaidi kuwa jenerali” kulingana na tajriba yake kubwa na sifa za kitaaluma.

Ruto alisema kuwa Ogolla baadaye alikiri kufanya "kosa" kwa madai ya kujaribu kuzuia ushindi wake katika uchaguzi.

"Nilikuwa na machaguo kumi. Ningeweza kumteua mtu yeyote, niliamua kinyume na ushauri wa watu wengi walioniambia 'usituze tabia ya aina hii'," Ruto alisema Mei 14 , 2023.

Mzunguko

Katika taifa la Afrika Mashariki, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi anachaguliwa miongoni mwa maafisa wakuu katika vitengo vya kijeshi vinavyohusika - jeshi, jeshi la wanamaji na jeshi la anga.

Nafasi ya Mkuu wa Majeshi ni ya mzunguko kati ya makamanda wa vitengo husika, ikimaanisha ikiwa mkuu wa jeshi la wanamaji atateuliwa CDF wakati huu, itakuwa zamu ya jeshi la anga au jeshi wakati ujao kutoa CDF.

Mara zote, nchi huwa na Mkuu mmoja tu wa Majeshi ya Ulinzi mwenye cheo cha Jenerali.

Ogolla, kamanda wa jeshi la anga, alikuwa amechukua nafasi ya Kibochi. Kabla ya uongozi wa Kibochi, kamanda wa jeshi la wanamaji, Samson Mwathethe, alikuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya.

TRT Afrika